Jumatano, 26 Januari 2022

JAJI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI MAKAO MAKUU MAHAKAMA YA TANZANIA

 Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, leo tarehe 26 Januari, 2022 ameweka jiwe la msingi kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yanayojengwa katika eneo la Tambuka Reli jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Prof. Juma ameishukuru Serikali la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha cha zaidi ya billioni 129 za Kitanzania ili kufanikisha mradi wa ujenzi huo.

“Napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha Mahakama kuweza kufikia katika hatua hii. Billioni 129 ni uwezeshaji mkubwa na tutaendelea kuuthamini siku zote,” alisema katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kwa sasa jengo la Makao Makuu ya Mahakama linalojumuisha Mahakama ya Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu (Majila Kuu) ambalo lipo katika eneo la mita za mraba 60, 000 linaonesha hatua nzuri iliyofikiwa, hivyo hakutakuwa na sababu yoyote ya kuacha kuhamia Dodoma wakati utakapofika.

Hivyo, amewataka Majaji, Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama kuanza kujiandaa kisaikolojia kwa ajili ya kuhamia Makao Makuu, huku akibainisha kuwa taarifa ya Matendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel inaonyesha shughuli za ujenzi zikamilika ifikapo Desemba 2022.

“Sasa tumefikia katika hatua ambayo kuhamia Dodoma hakukwepeki. Waheshimiwa Majaji tuanze kujitayarisha kisaikolojia, kama kujifunza lugha ya Kigogo tuanze kujifunza ili tuweze kujumuika na wananchi katika jiji hili kubwa la Dodoma,” ameseama.

Jaji Mkuu amesema kuwa muda wa kuwa tayari kukamilioka kwa ujenzi unafahamika, hivyo aliomba matayarisho ya kutoa huduma kuanza sasa. “Kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi sasa, siyo wakati jengo limekamilika ndiyo uanze kutafuta thamani na watumishi. Kwa hiyo matayarisho yaanze mapema ili kama tunaaza shughuli hapa baada ya siku ya sheria mwakani, basi hizo shughuli zianze,” amesema.

Amewashukuru wajenzi wanaosimamia ujenzi huo kwa hatua kubwa na ajabu iliyofikiwa na pia mihimili miwili ya Serikali na Bunge kwa kuendelea kuivumilia Mahakama kuendelea kubali Dar es Salaam katika kipindi chote cha matayarisho ya ujenzi na makazi ya Majaji yakiwa yanaendeelea.

Mhe. Prof. Juma amebainisha pia kuwa gharama iliyotumika katika mradi huo ni kubwa, hivyo akawataka watumishi wote wa Mahakama kulilinda na kulitunza jengo hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu na pia kwa manufaa ya wananchi kwa ujumla.

Hafla ya kuweka jewe la msingi katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Wilbert Martin Chuma pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Mahakama.

Baadhi ya viongozi kwa upande wa Serikali waliohudhuria waliongozwa na Waziri wa Sheria na Katiba, Mhe. George Simbachawene na Naibu Waziri, Mhe. Geofrey Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt Eliezer Mbuki Feleshi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Jumanne Sagini, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Khatibu Kazungu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Kiongozi Siyani amesema kuwa uwekaji wa jiwe la msingi wa jengo hilo hata kabla ya kukamilika kwake unatoa picha halisi ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, jambo ambalo lilisubiriwa siyo tu na watumishi wa Mahakama bali pia wananchi na wadau wote wa sheria nchini.

Amesema kuwa licha Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi, Mahakama ya Tanzania bado haina majengo yake maalumu kwa ajili ya Makao Makuu ambapo kumekuwepo na maafisa wengi mbalimbali wa Mahakama hulazimika kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma katika shughuli za kiserikali zinazohusisha mihimili mingine, jambo ambalo limekuwa likiongeza gharama za ofisi.

“Ni matumaini yangu kuwa kujengwa kwa jengo hili linalokusudiwa kutumika kama Makao Makuu  ya Mahakama hapa Dodoma kutaiwezesha Mahakama kuwa karibu na kuungana na mihimili mingine ya Serikali na hivyo kurahisisha mawasiliano na utendaji wa kazi baina yetu,” amesema Mhe. Siyani.

Jaji Kiongozi amebainisha pia kuwa uwekaji huo wa jiwe la msingi ni hatua nyingine katika uboreshaji unaoendelea katika Mahakama ya Tanzania ambayo ni matokeo ya mikakati iliyojiwekea kama Taasisi kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano (2015/16 – 2019/20), ambao mwaka huu umehuishwa kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano (2020/21 – 2024/25), na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama (2016/17 – 2020/21), ambao nao upo katika mchakato wa kuhuishwa, ili kukamilisha ujenzi wa mioundombinu unaoendelea sehemu mbalimbali pote nchini.

Kwa upande wake, Mhe. Simbachawene ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ya mfano. “Maeneo ambayo mnayasimamia na hasa kwenye miradi, kwa kweli mingi ni ya mfano, tunawapongeza sana,” amesema.

Amebainisha kuwa majengo mengi ambayo ataanza kuyatembelea wiki ijayo yanaonekana ni ya mfano. Kwa mujibu wa Waziri huyo, pamoja na kuwa na jukumu la kusimamia haki, Mahakama pia ina watu wazuri ambao wanaweza kusimamia miradi yao, hivyo alimpongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kusimamia vizuri kazi hizo.

Mhe. Simbachawene amebainisha pia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Samia Suluhu Hassan inayo dhamira na haijabadilisha chochote katika mwelekeo wa kuhakikisha Serikali kwa ujumla wake inahamia Dodoma na uwekezaji kubwa unaofanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania ni ishara kwa vitendo vya kuonyesha dhamira hiyo.

Mwonekano wa mbele wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yanayojengwa katika eneo la Tambuka Reli jijini Dodoma.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia)  akiweka jiwe la msingi kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yanayojengwa katika eneo la Tambuka Reli jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Sheria na Katiba, Mhe. George Simbachawene. Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 26 Januari, 2022.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza katika hafla ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa salamu fupi kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kuongea na wananchi katika hafla hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili katika eneo la ujenzi kwa ajili ya shughuli ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Waziri wa Sheria na Katiba, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi katika hafla hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  (katika waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji waliohudhuria hafla hiyo. Wengine waliokaa ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme (kulia kwa Jaji Mkuu) na Waziri wa Sheria na Katiba, Mhe. George Simbachawene na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Dkt Jabir Shekimweli (kushoto kwa Jaji Mkuu).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  (katika waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakandarasi wanaojenga jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  akiteta jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt Jaji Eliezere Mbuki Feleshi mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

(Picha na Innocent Kansha-Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni