Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa mwelekeo wa ujenzi wa Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania na kubainisha kuwa mradi huo unategemea kugharimu kiasi
cha shilingi za Kitanzania billioni 129.7.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo
la Makao Makuu ya Mahakama katika hafla ya kuweka jiwe la msingi iliyofanyika
jijini Dodoma leo tarehe 26 Januari, 2022, Prof. Ole Gabriel alimweleza Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni
rasmi kuwa katika gharama hizo hadi sasa wameshalipa billioni 47.2, sawa na
asilimia 36.3.
“Malipo haya yamekuwa yakifanyika
kwa muktadha unaofaa na kazi inaenda vizuri. Tunapenda kutoa shukrani za dhati kabisa
kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa fedha hizi zimekuwa
zikilipwa kwa wakati,” amesema Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama.
Amebainisha kuwa kazi za ujenzi katika
mradi huo zilianza Julai 2020, ambazo zitachukua miezi 30 na inategemewa kumalizika
tarehe 29 Desemba, 2022, ikiwa na maana kwamba
watumishi wa Mahakama watakuwa tayari tarehe 30 Decemba, kabla ya kumaliza
mwaka, kuingia kwenye jengo hilo. “Ikimpendeza Mungu Siku ya Sheria mwaka 2023
pengine kutakuwepo na jiwe la uzinduzi wa jengo hili,” amesema.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu, kwa miaka
mingi Mhimili wa Mahakama haukuwa na jengo la Makao Makuu, hivyo jitihada zilizianza
mwaka 2013, miaka tisa iliyopita na kwamba jengo hilo ilikuwa lijengwe katika
eneo la Chimala jijni Dar es Salaam, karibu kabisa na jengo refu lile
linalochungulia Ikulu ya Magogoni.
Amesema kuwa baada ya mipango ya
Serikali kuwa Makao Makuu ya nchi yanahamia Dodoma mchakato huo uligeuza
mwelekeo na ikaonekana jengo hilo lijengwe jijini Dodoma. Prof. Ole Gabriel
amesema kuwa mwaka 2017 mchakato huo ulipata msukumo pale ambapo Jaji Mkuu mwenyewe
ulipoongea na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt John Pombe Magufuli ili kuweza
kupata eneo jijini Dodoma.
“Baada ya hapo kasi iliongezeka
ambapo majadiliano yaliendelea na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu
(CDA) na baadaye Mamlaka ya jiji la Dodoma na eneo hili likapatikana na kwamba
Serikali ilielekeza Mahakama ipewe eneo la kutosha. Naomba kutoa taarifa kwamba
eneo ambalo tupo leo lina ukubwa wa hekta 18.9, takribani hekali 45 na eneo
hili hatujauziwa. Serikali ilielekeza Mahakama ipewe eneo hilo bure.
Tulishapata hati ya eneo hili kuweza kumuliki kwa miaka 99,” amesema.
Mtendaji Mkuu amewataja wanaosimamia
ujenzi ni CRJE, Kampuni ya Kichina ambao wanafanya kazi kubwa na kazi yao ni ya
viwango vya hali ya juu, huku akibainisha Wasanifu wa jengo hilo wakiwa ni Acquise
Achtectural Design ambao ni wazalendo.
Amebainisha pia kuwa jengo hilo lina
matawi matatu ambayo ni Mahakama ya Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani na
Mahakama Kuu. Prof. Ole Gabriel amemweleza Jaji Mkuu kuwa matawi hayo yanatengeneza
jengo katikati litakalokuwa linatumika kama ofisi za utawala. Amesema kuwa kati
ya billioni 129.7 za Kitanzania ambazo ni gharama ya jengo hilo, billioni 110
ndizo za ujenzi na billioni 19.7 ni kodi.
Akielezea maendeleo ya mradi huo,
Mtendaji Mkuu amesema kuwa katika ujenzi kuna hatua kubwa tano zinazojumuisha kuweka
msingi (Substructure), kusimamisha jengo lenyewe (Super structure) kuezeka (Roofing),
umaliziaji (Finishing) na mwisho ni kusawazisha eneo na kujenga ukuta (landscaping
and fencing).
Amesema kuwa ujenzi wa msingi umekamilika kwa kwa
asilimia 100, huku isimamishaji wa jengo ukifikia asilimia 99 katika jengo la Mahakama
ya Upeo na Mahakama ya Rufani, lakini kwenye jengo la Mahakama Kuu kazi hiyo ilishakamilika.
Mtendaji Mkuu amesema kuwa kazi ya umaliziaji
kwenye majengo yote itaaza muda sio mrefu mwezi wa pili na itakuwa kazi kubwa
ambayo itakwenda hadi mwezi Octoba, wakati kazi ya kusawazisha eneo na kujenga
ukuta itakuwa kazi ya mwisho. Amesema ukuta utakaojengwa una urefu wa mita
1700, hivyo ni jengo kubwa na lina mandhali nzuri sana.
Do you want to increase your website's domain authority (DA) score without using any black hat SEO technique then please read this link - https://how-to-increase-da-of-website-online.blogspot.com/
JibuFuta