Jumatano, 26 Januari 2022

WATUMISHI WA MAHAKAMA KANDA YA SONGEA WATOA MSAADA KWA YATIMA

MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA NCHINI, 2022

Na Brian Haule, Mahakama-Songea

Mahakama ya Tanzania ipo katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, katika maadhimisho haya Mahakama nchini zinaadhimisha kwa kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli mbalimbali zinazogusa jamii ikiwemo kutoa misaada kwa wagonjwa, watoto yatima kama walivyofanya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Songea waliotembelea na kutoa msaada katika Kituo cha kulea Watoto yatima mnamo tarehe 25 Januari, 2022.

Watumishi hao walioongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe.Livin Benedict Lyakinana walitembelea Kituo cha ‘St. Anthony Orphanage’ kilichopo maeneo ya Mfaranyaki Manispaa ya Songea.

Miongoni mwa misaada waliyotoa kwa ajili ya Watoto yatima wa kituo hicho ni pamoja na Mchele, Mafuta ya Kupikia, Unga na Mbuzi kwa Uongozi wa Kituo hicho.

Akiongea kwa niaba ya Uongozi wa Kituo cha kulelea yatima cha Mtakatifu Anthony, Sista Judith Mwageni ameshukuru Uongozi wa Mahakama Kanda ya Songea kwa kuwatembelea na kuwapatia mahitaji ambayo yatawasaidia kuhudumia Watoto katika kituo hicho.

Akiongea kwa niaba ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Songea, Mhe. Lilian Haule Hakimu Mkazi alisema Watumishi wa Mahakama wamefurahi kutembelea kituo hicho kwani watoto hao ni sehemu ya familia yao na ni wajibu wao kuwasaidia, vilevile aliwahimiza Watoto hao kusoma kwa bidii ili elimu hiyo iweze kuwasaidia katika maisha yao hapo baadae.

Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Livin Benedict Lyakinana  (kulia) akikabidhi mbuzi kwa Sista Judith Mwageni upande wa kushoto ambaye ni mlezi wa watoto katika kituo cha yatima cha Mtakatifu Anthony. Misaada hiyo ilitolewa Watumishi wa Mahakama Kanda ya Songea tarehe 25 Januari, 2022.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni