Jumatano, 26 Januari 2022

BALOZI KATTANGA ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA SHERIA DODOMA

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga ametembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma ambapo ameipongeza Mahakama kwa uboreshaji wa huduma huku akishauri kuhusisha wanafunzi katika matukio mbalimbali ili kuwapa hamasa ya kuipenda fani ya sheria.

Akizungumza mara baada ya kukagua mabanda kadhaa yaliyopo katika Maonesho hayo tarehe 26 Januari, 2022, Balozi Kattanga alisema kuwa amefurahi kuwa Mahakama imepiga hatua katika uboreshaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa.

“Nina furaha kuwa katika kipindi cha takribani miaka mitatu (3) niliyotoka mahakamani naona kuna mabadiliko makubwa ambayo yametokea hususani upande wa mifumo ya TEHAMA. Hata hivyo naomba utaratibu wa kuwahusisha Wanafunzi wa shule mbalimbali uendelee ili kuwajenga Watoto kuipenda fani ya sheria bado mapema,” alisema Balozi Kattanga.

Aidha; Katibu Mkuu Kiongozi ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mhimili wa Mahakama ili kuuwezesha Mhimili huo wa Mahakama kuendelea kutoa haki kwa wananchi.

Balozi Kattanga alipata pia fursa ya kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma na vilevile kukagua Mradi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yanayojengwa katika eneo la Tambuka reli jijini Dodoma ambapo pia ameonyesha kufurahishwa na ubora wa jengo la 'IJC' Dodoma na hatua kubwa iliyofikiwa ya mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Mahakama.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa kutenga muda wake na kuamua kuja kutembelea maonesho hayo, kutembelea jengo la 'IJC' na kukagua mradi wa ujenzi wa Makao makuu ya Mahakama.

"Nikiri wazi kuwa nimefurahishwa na ujio wako Mhe. Balozi Kattanga, na tunashukuru kwa ushirikiano ambao Serikali inaendelea kutupa, kutuwezesha kutimiza ili malengo yetu, tunaahidi kuendelea kuboresha huduma na kuendeleza mazuri yote uliyoyaacha ukiwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama," alisema Prof. Ole Gabriel.

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga (kushoto) akipata maelezo kuhusu masuala ya Mirathi kutoka kwa Mtumishi wa Mahakama. Mhe. Balozi Kattanga ametembelea katika Maonesho ya Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma tarehe 26 Januari, 2022.


Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga (kushoto)  akipata maelezo kutoka kwa Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wakati alipotembelea mabanda yaliyopo katika Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini katika Viwanja vya Nyerere 'Square' Dodoma.

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga (kulia) akisoma kipeperushi alipotembelea moja ya mabanda ya Wadau wa Mahakama yaliyopo katika Viwanja vya Nyerere 'Square' Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akijadili jambo na Mhe. Balozi Kattanga wakati Balozi huyo alipotembelea Mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini, 2022.

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga (kulia) akifurahia jambo na Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Enziel Mtei (kushoto) wakati alipotembelea na kupata maelezo kutoka kwa Bi. Mtei.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Jaji Mstaafu Joaquine De Mello (kushoto) akitoa maelezo kuhusu Chama hicho wakati Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga alipotembelea banda la TAWJA.
Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga akisaini vitabu vya wageni alipowasili katika Maonesho ya Wiki ya Sheria Viwanja vya Nyerere 'Square' Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyenyoosha mikono) akimuongoza Mhe. Balozi Hussein Kattanga (wa pili kulia) kukagua Mradi wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Msanifu Majengo kutoka Chuo cha Ardhi, Bi. Rose akimuonyesha Mhe. Balozi Kattanga mchoro ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama.
Maelezo kuhusu Mradi wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yakitolewa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga (wa pili kushoto). Wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 'IJC' Dodoma, Mhe. Jaji Mdemu, wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
 
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


 


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni