Alhamisi, 27 Januari 2022

JAJI MKUU AHIMIZA MATUMIZI YA MIFUMO INAYONUFAISHA WANANCHI

 Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezihimiza taasisi mbalimbali za utoaji haki nchini kutumia mifumo ya kisasa itakayowawezesha wananchi kupata huduma kwa haraka, hivyo kuchochea ustawi wa kiuchumi na maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla.

Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 27 Januari, 2022 alipotembelea mabanda ya maonesho yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea.

“Lazima tupige hatua zaidi ili hii mifumo ya kila taasisi izungumze, isaidia uchumi na isaidia wananchi waweze kupata huduma huko huko walipo,” amesema alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea madanda hayo.

Jaji Mkuu aliyefuatana na viongozi mbalimbali, akiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Siyani na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme, amesema kuwa kitu kimoja ambacho amejifunza katika mabanda hayo ni kuona taasisi zinazotoa haki au zilizo katika mnyororo wa sheria zinafanya kazi kubwa katika kuwahudumia wananchi.

Amebaini pia kuwa kuna nyaraka nyingi ambazo zinaonesha kazi mbalimbali zinazofanywa na taasisi hizo na kwamba mabanda mengi yamefunga na kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli zao za kila siku za utoaji haki.

Hata hivyo, Mhe, Prof. Juma amebaini mifumo inayotumiwa na taasisi hizo haiongei kwa manufaa ya wananchi, jambo ambalo ni changamoto kuelekea kwenye safari ya zama za mapinduzi ya nne ya viwanda. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kila mfumo umesimama pekee yake.

“Unaweza kukuta Mahakama wana mifumo mizuri na wanatoa huduma kwa kutumia TEHAMA. Ukienda Wizara ya Ardhi nao wana mifumo, hivyo kila mmoja ana mifumo, lakini hii mifumo haizungumzi kwa manufaa ya wananchi. Kwa hiyo, kwa miaka minne ijayo kabla hatujamaliza robo ya kwanza ya karne ya 21, ni wakati wa kufanya mifumo yetu izungumze,” amesema.

Ametoa mfano mfumo katika Wizara ya Ardhi kuhusu utoaji taarifa ambapo unaweza kukuta unatumika zaidi kurahisisha kazi za Wizara, kusaidia kutoa huduma, lakini ukiangalia nchi nyingine ambazo zina mifumo ya ardhi imelenga katika kuwasaidia wananchi.

“Kwa mfano, mwekezaji anataka kujua taarifa ya ardhi iliyopo Kigoma na yeye yupo Dar es Salaam, kwa hiyo mifumo hiyo inatakiwa impe taarifa zote bila kuwa na haja ya kuja ofisini,” amesema Jaji Mkuu.

Ameeleza pia kuwa nchi ya Kenya ina mifumo mizuri inayoitwa Ardhi Sasa, ambayo hawaitumii kwa ajili ya kukusanya pango tu, bali pia kurahisisha utoaji wa huduma. Amesema kuwa mashauri mengi ambayo wanapokea mahakamani kuhusu masuala ya ardhi yanatakiwa yawe yametatuliwa na Kamishna wa Ardhi, na siyo kuja mahakamani.

“Unakuta wananchi wanakuja mahakamani na kila mmoja wao anasema ana haki kwenye kipande cha ardhi, lakini mwenye taarifa hizo ni Kamishna wa Ardhi. Kwa nini asiwe na mfumo ambao unamaliza hizo changamoto na kuzileta mahakamani halafu Mahakama ndiyo itoe amri kwamba hii ardhi ni ya nani,” amesema.

Kwa hiyo ameshauri pamoja na kuwepo mifumo hiyo mizuri lazima kupiga hatua mbele zaidi ili iweze kuzungumza, isaidia uchumi na isaidia wananchi waweze kupata huduma huko huko walipo.

“Hilo ni jambo moja ambalo nadhani liwe mtihani kwetu kwa hii miaka mitano ijayo. Mnakumbuka hii karne ilipoanza, Rais wakati huo alikuwa Benjamin Mkapa na katika lile toleao la Dira ya Taifa ya Maendeleo alisema karne ya 21 ni karne ya ushindani na atakayeshinda kwenye ushindani huo ni yule mwenye teknolojia ya kisasa,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, kwa sasa Watanzania wamebakiza miaka minne kukamilisha hiyo robo ya kwanza, lakini kabla ya kufikia hiyo dira ya pili lazima kuwa tayari na wawe wameingia katika mashindano ya teknolojia.

“Ndiyo maana katika mwaka huu tunasema katika safari yetu tuwe na Mahakama Mtandao itakapofika hiyo tarehe 31 Desemba, 2025  na tuwe ni nchi inayoshidana na nchi yoyote katika masuala ya tekinolojia katika utoaji haki,” amesema.

Mahakama ya Tanzania imeandaa Wiki ya Sheria inayoadhimishwa kote nchini. Maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa jijini Dodoma. Jumla ya mabanda 46 yameandaliwa kutoa elimu na huduma mbalimbali za kisheria katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Kati ya hayo, mabanda ya Mahakama yapo saba, huku yaliyobaki 39 ni ya wadau mbalimbali wa Mahakama.

Kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, Jaji Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali, ikiwepo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama pamoja na mengine ambapo amejionea shughuli na huduma kadhaa zinazotolewa.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimweleza jambo Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock (wa pili kushoto) alipotembelea banda lao leo tarehe 27 Januari, 2022 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari leo tarehe 27 Januari, 2022 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifafanua umuhimu wa teknolojia alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari. Kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Siyani na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimsikiliza mmoja wa maafisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipotembelea banda lao.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea moja ya nyaraka kutoka kwa kiongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe Shamillah Sarwatt, ambaye pia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alipotembelea banda lao.

Mmoja ya maafisa kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria akitoa maelezo kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipotembelea banda lao leo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. 


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiangalia zawadi aliyokabidhiwa katika banda la Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU). 


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bw. Abubakar Mrisha akimweleza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma shughuli mbalimbali zinazofanywa  na Ofisi ya Wakili Mkuu alipotembelea banda hilo.

Jaji Mkuu wa Tanzania akipokea maelezo kutoka kwa afisa wa Mahakama ya Tanzania alipotembelea banda la Mirathi.

Mmoja wa maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi akimkabidhi Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma moja ya nyaraka alipotembelea banda lao.

Wakili wa Kujitegemea Mwandamizi, Msomi Deus Juma Nyabiri  akimweleza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma shughuli mbalimbali zinazofanywa na Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) alipotembelea banda hilo.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea maelezo ya shughuli mbalimbali kutoka kwa afisa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati)kakipokea maelezo kutoka kwa Katibu wa Kamati Kuu ya Maandalizi ya Wiki ya Sheria, Mhe. Charles Magesa (wa kwanza kulia) alipowasili katika viwanja vya Nyerere Square kukagua mabanda mbalimbali.

                                                (Picha na Innocent Kansha-Mahakama)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni