Na Magreth
Kinabo- Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Dar es
Salaam Mhe. Amir Mruma leo tarehe 27 Januari, mwaka
2022 amefungua mafunzo ya elimu ya sheria kwa watendaji wa kata wa mkoa wa Dar
es Salaam ili kuwajengea uwezo wa kutatua migogoro ya kijamii kama vile ndoa,
talaka na mirathi.
Akizungumza na watendaji kata hao, katika ukumbi wa Manispaa
ya Temeke, Jaji Mruma alisema elimu hiyo, imetolewa ikiwa ni mwendelezo wa
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika kanda hiyo.
‘‘Nyie ni wadau wetu wa Mahakama, pia ni walinzi wa
amani katika maeneo yenu, sisi na nyie tunafanya kazi ya kuhakikisha nchi yetu
ina amani, hivyo tutaendelea kushirikiana,’’ alisema Jaji Mruma.
Jaji Mruma aliongeza kwamba hivi sasa Mahakama inatoa
haki kwa njia ya mtandao, hivyo haitarudi nyuma, bali itatengeneza mfumo wa
kuweza kuwasiliana na nyie.
Kwa upande wake
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Ramadhani Rugemalila, alisema wametoa mafunzo
hayo ili kuweza kuwafanya watendaji hao kuwa wasuluhishi wazuri juu ya migogoro
hiyo inayoibuka katika jamii kupitia barazala usuluhishi. Mafunzo hayo
yamehusisha watendaji kata zaidi ya 100.
Naye Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)cha
masuala ya kifamilia, Mhe. Ilvin Mugeta, akitoa mada ya Sheria ya Ndoa alisema ni vizuri watendaji hao kuwa wasiri,
wasio na upendeleo,na kuzingatia maadili ,ikiwemo kutopokea rushwa wanapoifanya
kazi hiyo ya usuluhishi.
Jaji Mugeta pia aliwataka watendaji hao kuzingatia
ujazaji mzuri wa fomu namba tatu ya usuluhishi, pale baraza la usuluhishi
linaposhindwa kutatua mgogoro wa ndoa.
Akizungumzia kuhusu IJC Jaji Mugeta alisema tangu kianzishwe tarehe 27 Agosti kimeshapokea mashauri 2,044, hivyo aliwataka watu wenye migogoro kuhusu masuala ya ndoa wafike katika kituo ili kuweza kupata haki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni