Jumatano, 26 Januari 2022

UJENZI MAKAO MAKUU MAHAKAMA YA TANZANIA KUGHARIMU BILLIONI 129: MTENDAJI MKUU

 Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa mwelekeo wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na kubainisha kuwa mradi huo unategemea kugharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania billioni 129.7.

Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama katika hafla ya kuweka jiwe la msingi iliyofanyika jijini Dodoma leo tarehe 26 Januari, 2022, Prof. Ole Gabriel alimweleza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kuwa katika gharama hizo hadi sasa wameshalipa billioni 47.2, sawa na asilimia 36.3.

“Malipo haya yamekuwa yakifanyika kwa muktadha unaofaa na kazi inaenda vizuri. Tunapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa fedha hizi zimekuwa zikilipwa kwa wakati,” amesema Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama.

Amebainisha kuwa kazi za ujenzi katika mradi huo zilianza Julai 2020, ambazo zitachukua miezi 30 na inategemewa kumalizika tarehe 29 Desemba, 2022, ikiwa na  maana kwamba watumishi wa Mahakama watakuwa tayari tarehe 30 Decemba, kabla ya kumaliza mwaka, kuingia kwenye jengo hilo. “Ikimpendeza Mungu Siku ya Sheria mwaka 2023 pengine kutakuwepo na jiwe la uzinduzi wa jengo hili,” amesema.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu, kwa miaka mingi Mhimili wa Mahakama haukuwa na jengo la Makao Makuu, hivyo jitihada zilizianza mwaka 2013, miaka tisa iliyopita na kwamba jengo hilo ilikuwa lijengwe katika eneo la Chimala jijni Dar es Salaam, karibu kabisa na jengo refu lile linalochungulia Ikulu ya Magogoni.

Amesema kuwa baada ya mipango ya Serikali kuwa Makao Makuu ya nchi yanahamia Dodoma mchakato huo uligeuza mwelekeo na ikaonekana jengo hilo lijengwe jijini Dodoma. Prof. Ole Gabriel amesema kuwa mwaka 2017 mchakato huo ulipata msukumo pale ambapo Jaji Mkuu mwenyewe ulipoongea na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt John Pombe Magufuli ili kuweza kupata eneo jijini Dodoma.

“Baada ya hapo kasi iliongezeka ambapo majadiliano yaliendelea na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na baadaye Mamlaka ya jiji la Dodoma na eneo hili likapatikana na kwamba Serikali ilielekeza Mahakama ipewe eneo la kutosha. Naomba kutoa taarifa kwamba eneo ambalo tupo leo lina ukubwa wa hekta 18.9, takribani hekali 45 na eneo hili hatujauziwa. Serikali ilielekeza Mahakama ipewe eneo hilo bure. Tulishapata hati ya eneo hili kuweza kumuliki kwa miaka 99,” amesema.

Mtendaji Mkuu amewataja wanaosimamia ujenzi ni CRJE, Kampuni ya Kichina ambao wanafanya kazi kubwa na kazi yao ni ya viwango vya hali ya juu, huku akibainisha Wasanifu wa jengo hilo wakiwa ni Acquise Achtectural Design ambao ni wazalendo.

Amebainisha pia kuwa jengo hilo lina matawi matatu ambayo ni Mahakama ya Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu. Prof. Ole Gabriel amemweleza Jaji Mkuu kuwa matawi hayo yanatengeneza jengo katikati litakalokuwa linatumika kama ofisi za utawala. Amesema kuwa kati ya billioni 129.7 za Kitanzania ambazo ni gharama ya jengo hilo, billioni 110 ndizo za ujenzi na billioni 19.7 ni kodi.

Akielezea maendeleo ya mradi huo, Mtendaji Mkuu amesema kuwa katika ujenzi kuna hatua kubwa tano zinazojumuisha kuweka msingi (Substructure), kusimamisha jengo lenyewe (Super structure) kuezeka (Roofing), umaliziaji (Finishing) na mwisho ni kusawazisha eneo na kujenga ukuta (landscaping and fencing).

 Amesema kuwa ujenzi wa msingi umekamilika kwa kwa asilimia 100, huku isimamishaji wa jengo ukifikia asilimia 99 katika jengo la Mahakama ya Upeo na Mahakama ya Rufani, lakini kwenye jengo la Mahakama Kuu kazi hiyo ilishakamilika. 

Mtendaji Mkuu amesema kuwa kazi ya umaliziaji kwenye majengo yote itaaza muda sio mrefu mwezi wa pili na itakuwa kazi kubwa ambayo itakwenda hadi mwezi Octoba, wakati kazi ya kusawazisha eneo na kujenga ukuta itakuwa kazi ya mwisho. Amesema ukuta utakaojengwa una urefu wa mita 1700, hivyo ni jengo kubwa na lina mandhali nzuri sana.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa taarifa ya ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo linalojengwa jijini Dodoma. Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 26 Januari, 2022 ambapo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alikuwa mgeni rasmi.
Meza kuu inayojumlisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kulia) ikimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo kwenye picha) wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania. Kulia kwa Jaji Mkuu ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ambaye anafuatiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme. Kushoto kwa Jaji Mkuu ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe George Simbachawene.
Mwonekano wa mbele wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania linalojengwa jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili katika eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongea na wananchi katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  (katika waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakandarasi wanaojenga jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akisalimiana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe George Simbachawene walipokutana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akimweleza jambo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe George Simbachawene.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme (katikati) akiangalia mandhali ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania. Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma na kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiondoka katika eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania mara baada ya kuweka jiwe la msingi, huku akisindikizwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma (kushoto).




Mmoja wa viongozi wa kampuni ya Wasanifu wa jengo hilo (aliyeshika kijiti) akimwelezea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kushoto) namna ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania unavyotekelezwa.
(Picha na Innocent Kansha-Mahakama

Maoni 1 :

  1. Do you want to increase your website's domain authority (DA) score without using any black hat SEO technique then please read this link - https://how-to-increase-da-of-website-online.blogspot.com/

    JibuFuta