Na Mary Gwera, Mahakama
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Sichwale ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuchukua hatua ya kuhamasisha mapambano dhidi ya UVIKO-19 ikiwemo watumishi wake kushiriki katika zoezi la chanjo linaloendelea kote nchini.
Dkt Sichwale ametoa pongezi hizo leo tarehe 24 Januari, 2022 wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa Nyaraka za Mahakama na Hamasa ya chanjo ya UVIKO 19 uliofanyika katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
“Mhe. Jaji Mkuu kwanza nikupongeze wewe binafsi na watendaji katika Ofisi yako kwa maandalizi na niwashukuru sana kwa kuona umuhimu wa kutenga siku ya leo kuwa siku ya kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu suala la ugonjwa wa UVIKO na umuhimu wa kupata chanjo kwa watumishi wa Mahakama, huu ni mfano wa kuigwa na taasisi zingine kwani ugonjwa bado upo,” alisema.
Dr. Sichwale alisema kuwa Wizara ya Afya ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Mahakama ili kuwezesha Watumishi wake kupata chanjo ili kuendelea kupambana na UVIKO 19.
Aliongeza kwa kutoa angalizo kuwa ugonjwa wa Covid bado upo, hivyo chanjo ni muhimu na kuendelea kuchukua tahadhari nyingine ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na uvaaji wa barakoa katika maeneo yenye misongamano.
Alisema kuwa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliporidhia matumizi ya chanjo nchini, Tanzania imeendelea kupokea na kutoa chanjo kwa wananchi kupitia njia mbalimbali.
Amebainisha kuwa hadi kufikia tarehe 23 Januari, 2022, jumla ya dozi 3,423,563 kati ya dozi 6,408,950, sawa na asilimia 61 zilizopokelewa zilikuwa zimetolewa kwa wananchi, ambapo idadi ya waliopata dozi kamili mpaka kufikia tarehe 23 Januari, 2022 kwa Tanzania Bara na Visiwani ni asilimia 3.27.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma alisema kuwa kulingana na uzoefu aliouona kuhusu UVIKO, maambukizi hupanda na kushuka, hivyo inabidi kuendelea kujifunza kuishi kwa tahadhari siku zote maana athari zake zitaendelea kujitokeza sana.
“Hakuna nchi yoyote duniani ambayo ilijitayarisha kukabiliana na janga la Uviko-19. Janga hili lilijitokeza ghafla na kusambaa kwa kasi kubwa. Janga hili limebadili kabisa maisha yetu, namna tunavyohusiana na binadamu wenzetu tunaoishi nao, tunaofanya nao kazi, tunaotoa huduma kwao. Lazima tujipongeze namna tulivyoweza kubadilika kutoka kuwa waoga na kuogopana, hadi kuweza kuendelea kuishi Pamoja na kuendelea kutoa huduma tukiwa pamoja,” alisema Mhe. Prof. Juma.
Aliongeza kwa kuwataka Watumishi wa Mahakama kuchukua tahadhari zote zinazoshauriwa na Wizara ya afya ikiwemo kuchanja.
“Sisi watumishi wa Mahakama na pia wadau wa Mahakama, wananchi wanaofuata huduma za Mahakama tuna jukumu endelevu la kuendelea kijifunza namna mbali mbali za maambukizi, namna ugonjwa unavyosambaa, tahadhari tunazotakiwa kuzichukua, tahadhari za kujilinda na kuwalinda wenzetu tunaofanya nao kazi,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Hata hivyo; Mhe. Jaji Mkuu alisisitiza juu ya matumizi ya TEHAMA katika kazi, akitoa mfano wa janga la UVIKO lilivyoingia bado Mahakama ya Tanzania iliendelea kutoa huduma kwa kuongeza matumizi ya teknolojia katika kusajili mashauri, usikilizwaji wa mashauri, matumizi ya e-mails katika mawasiliano, kuwawezesha watumiaji wa Mahakama kupata taarifa zao muhimu kupitia Tovuti ya Mahakama pamoja na matumizi ‘Video Conference’.
Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amesema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa tangu mlipuko wa maambukizi ya UVIKO 19 hadi sasa, wamepitia changamoto nyingi ambazo sio tu zinaathiri afya za watumishi bali pia utendaji kazi. Hata hivyo, alisema kuwa changamoto hiyo imeleta pia mchango chanya katika utendaji wa kazi.
“Utakumbuka Mhe. Jaji Mkuu, awali, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Korona, Mahakama ilikuwa aidha ifunge huduma zake kwa kuwalinda watumishi na wadau kwa ujumla au ije na mkakati utakaowezesha usikilizwaji wa Mashauri bila kuhatarisha Maisha ya watumishi na wadau kwa ujumla,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, kwa bahati nzuri, Mahakama ilikuwa tayari ina msingi mzuri wa kukabiliana na changamoto ya korona kutokana na uwepo kwa Mpango Mkakati wa Mahakama (Judiciary’s Five – Year Strategic Plan and the Citizens Centric Judicial Modernization and Justice Service Delivery Project) ambao ulijumuisha maboresho ya miundombinu ya huduma za TEHAMA iliyoisadia Mahakama kukabiliana na athari za ugonjwa wa Korona kwani programu ya Mashauri Mtandaoni (JSDS 2) inajumuisha pia 'E – Judiciary'. Programu husika iliwezesha kusikiliza Mashauri kwa mtandao bila ulazima wa uwepo wa wadau.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma akishuhudia mmoja kati ya Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania waliojitokeza kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 baada ya kupata elimu ya uhamasishaji kutoka kwa viongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya. Zoezi hili la uchanjaji limefanyika leo tarehe 24 Januari, 2022 wakati wa uzinduzi wa Nyaraka za Mahakama na Hamasa ya chanjo ya UVIKO 19 uliofanyika katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Sichwale akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa Nyaraka za Mahakama na Hamasa ya chanjo ya UVIKO 19 uliofanyika leo tarehe 24 Januari, 2022 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma akitoa hotuba leo katika Viwanja vya Nyerere Square mjini Dodoma kabla ya uzinduzi wa Majuzuu na kuhamasisha kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania na wananchi.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wananchi wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim khamis Juma (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa hotuba ya uzinduzi wa Majuzuu ya Sheria na kuhamasisha watumishi wa Mahakama kushiriki chanjo ya kujinga na UVIKO 19.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa maelezo ya utangulizi leo kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Taanzania Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma(hayupo katika picha ) kwa ajili ya kuhutubia na kisha azindue majuzuu ya kisheria kwenye Viwanja vya Nyerere Square mjini Dodoma.
Baadhi ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) baada ya kuzindua Majuzuu ya Sheria na kampeni ya kuhamasisha watumishi wa Mahakama kuchanja chanjo ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Sheria ambayo kitaifa yanaendelea katika Viwanja vya Nyerere Squares Mjini Dodoma mpaka tarehe 29 Januari, 2022.
Kwaya ya Mahakama ya Tanzania ikitumbuiza leo wakati wa uzinduzi wa Nyaraka za Mahakama na Hamasa ya chanjo ya UVIKO 19.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni