Na Faustine Kapama, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma, leo tarehe 24 Januari, 2022 amezindua Majuzuu ya Taarifa za
Sheria Tanzania kwa Mwaka 2007 hadi 2020 yanayojumuisha maamuzi ya Mahakama Kuu
(Tanzania), Mahakama Kuu (Zanzibar) na Mahakama ya Rufani, tukio ambalo ni muhimu
katika utoaji haki kwa wananchi.
Hatua hiyo ilienda sambamba na
uzinduzi wa Faharisi (Index) ya Sheria Mama na Sheria ndogo za kuanzia Mwaka
1961-2020, vyote vikiwa katika mfumo wa nakala laini na nakala ngumu, jambo
ambalo limelenga kuwasaidia maafisa wa Mahakama na Wadau kutumia vitabu vya taarifa
hizo za sheria katika kusimamia utoaji haki.
Sanjali na tukio hilo muhimu, Mhe.
Prof. Juma pia alizindua mfumo wa kielektroniki (e-Wakili Management System)
mara baada ya kupokea maelezo mafupi kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt, mfumo mpya ambao umeanzishwa mahususi kwa
ajili ya kusajili, kutunza kumbukumbu na kuratibu leseni za Mawakili pamoja na
taratibu zote zinazowahusu, mara baada ya mfumo uliokuwa unatumika hapo awali
kuwa na changamoto kadhaa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji
Mkuu alibainisha kuwa hiyo ni mara ya tatu machapisho hayo yameweza kutolewa na
Mahakama ya Tanzania ambapo Chapisho la kwanza lilikuwa la mwaka 1980-1996 na Chapisho
la pili lilikuwa la mwaka 1997-2006. Amesema kuwa uamuzi wa mashauri mengi katika
Chapisho la tatu utaonekana kuwa ni wa Mahakama ya Rufani ikiwa ni muendelezo
wa kutoa nakala zingine za uamuzi wa Mahakama Kuu (T) na Zanzibar katika kila
mwaka husika kuwa na chapisho la pili (Volume II - Supplementary Volume).
“Hii inatokana na Mahakama ya
Tanzania kupiga hatua kubwa ya upatikanaji wa uamuzi katika nakala laini kupitia
Maktaba Mtandao na TanzLII, hivyo kuwezesha kuilisha Bodi ya Uhariri uamuzi katika
mashauri mengi kwa mwezi ikiwa ni takribani ya uamuzi wa mashauri 600 hadi 700,”
amesema.
Hata hivyo, Mhe. Prof. Juma alieleza
kuwa machapisho ya mwanzo kabla ya uhuru yalianza Mwaka 1921 wakati Mahakama
Kuu ya Tanganyika inaanza shughuli zake tarehe 3 Januari, 1921 ambapo uamuzi katika
mashauri mengi katika kipindi hicho ulitolewa taarifa kati ya mwaka 1921 hadi
1952 ambayo iliitwa (Tanganyika Territory Law Reports), hii ikiwa ni chapisho
la kwanza.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, mwaka 1953
hadi 1957 kulikuwa na chapisho la pili na baadae kuwa na chapisho la tatu mwaka
1958 hadi 1966. Amesema kuwa katika mwaka 1967 hadi mwaka 1972 machapisho ya
makusanyiko ya uamuzi wa Mahakama Kuu ulitolewa (High Court Digests 1967-1972)
na mwaka 1973 hadi mwaka 1979 Taarifa za Majuzuu zilitolewa (The Law Reports of
Tanzania 1973-1979) kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mhe. Prof. Juma ameendelea kueleza
kuwa baadae kuanzia mwaka 1980, Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria
ilibadilika na kuwa na uenyekiti kupitia Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Barnabas
Samatta na kuanzia kipindi hicho Mahakama ya Tanzania iliendelea na
shughuli za uchapaji wa machapisho yote.
“Naomba nitoe pongezi na shukrani
kwa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa ufadhili kwa
Mahakama ya Tanzania kwa kuwezesha na kufanikisha matoleo yote haya ya majuzuu
(vitabu) vya miaka yote 14 na Faharisi za
Sheria Mama na Sheria ndogo za kuanzia Mwaka 1961-2020, vyote vikiwa katika
mfumo wa nakala laini na nakala ngumu. Wao wamekuwa wadau wakubwa wa utoaji
haki katika mashauri katika ngazi zote za Mahakama na wamekuwa wanasaidia
Mahakama ya Tanzania katika mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa utoaji
haki,” amesema.
Jaji Mkuu amesema kuwa Mahakama
itaendelea kuimarisha upatikanaji wa nakala za maamuzi na Taarifa za Majuzuu ya
Sheria Tanzania kwa miaka ya nyuma kuanzia Mwaka 1980 hadi Mwaka 2006. Aidha ameomba
Mahakama kupitia Idara ya Menejimenti ya Mashauri na Kitengo cha Maktaba
kuendeleza utaratibu huo wa kuandaa Faharisi ya Sheria Mama na Sheria ndogo kwa
Mwaka 2021 na kuendelea.
Kwa upande wake, Jaji kiongozi wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe, Mustapher Siyani amesema kuwa Majuzuu ya Taarifa za
Sheria ni nyenzo muhimu za kazi kwa kila mwana taaluma wa sheria ambapo kutoka
katika taarifa hizo uamuzi wa mashauri mbalimbali yanayoakisi msimamo au
mwelekeo wa sheria katika nchi yetu hupatikana.
Amesema kuwa taarifa hizo huwasaidia
wananchi na Mawakili wanaofika mahakamani kila siku kutafuta haki kujua
misimamo mbalimbali ya kisheria kupitia uamuzi ya Mahakama za juu. Aidha,
amesema kuwa kwa Majaji na Mahakimu, Majuzuu hayo ya Taarifa za Sheria ni rejea
ya kila siku kwani agalabu kwa maafisa hao wa Mahakama hufanya uamuzi bila
kurejea uamuzi mwingine uliowahi kufanywa kwenye eneo husika, ikiwa upo.
“Umuhimu wa machapisho wa Majuzuu ya
Taarifa za Sheria ulianza kuonekana tokea zama za ukoloni kabla ya uhuru wa nchi
yetu ambapo kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 2020 kwa vipindi tofauti kulitolewa
machapisho matatu yakifuatiwa na machapisho kadhaa yaliyorejewa kama High Court
Digest, Law Reports of Tanzania na
baadaye Tanzania Law Reports,” amesema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mratibu wa Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria Tanzania, Mhe Kifungo Mrisho amesema kuwa katika kupatikana kwa machapisho hayo kumekuwepo na mchakato mwingi, ikiwemo kuingia katika Mahakama Mtandao na masuala ya TEHAMA ili kuwezesha kupata uamuzi wa mashauri mengi ya Mahakama Kuu (Tanzania), Mahakama Kuu (Zanzibar) na Mahakama ya Rufani, hatua ambayo imewezesha taarifa zote kuanzia mwaka 2007 hadi 2020, takribani miaka 14 kuweza kupatikana.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo
yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri wa Majuzuu
ya Taarifa za Sheria, Mhe. Jacobs Mwambegele, Jaji wa Mahakama ya Rufani,
ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na timu yote
ya wajumbe iliyowezesha taarifa hizi kupatikana, bila kusahau ushirikiano
walioupata kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel na
kitendo cha uboreshaji wa huduma mbalimbali cha Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizindua Majuzuu ya Taarifa za Sheria Tanzania kwa Mwaka 2007 hadi 2020 katika hafla iliyofanyika leo tarehe 24 Januari, 2022 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Wanaoshuhudia uzinduzi huo ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (wa kwanza kushoto), Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt Aifello Sichwale (kulia kwa Jaji Mkuu) na viongozi wengine.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akionyesha wananchi waliofurika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma (hawapo katika picha) nakala ya Majuzuu ya Taarifa za Sheria Tanzania kwa Mwaka 2007 hadi 2020 mara baada ya kuzizindua leo tarehe 24 Januari, 2022. Kiongozi wa kwanza kutoka kushoto kwa Jaji Mkuu ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria, Mhe. Jacobs Mwambegele, Jaji wa Mahakama ya Rufani, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, anafuatiwa na Naibu Mratibu wa Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria Tanzania, Mhe Kifungo Mrisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni