Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Lubigija Ng’wilabuzu, ameiomba Mahakama ya Tanzania kuondoa kesi zisizokuwa na ushahidi mahakamani, isipokuwa zile zenye mazingira ya kiusalama, mfano kuua au kubaka ili kuweza kupunguza mlundikano wa mahabusu magerezani.
Bw. Ng'wilabuzu, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, ametoa ombi hilo leo tarehe 23 Januari, 2022 baada ya kushiriki katika matembezi ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ulioandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.Matembezi hayo yalianzia Mahakama Kuu ya Tanzania mpaka mahakama hiyo.
Ameviomba vyombo husika kushirikiana na Mahakama
kuziondoa kesi hizo kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya mahabusu katika magereza.
‘‘Uondoshaji wa mashauri haya yasiyokuwa na ushahidi mahakamani
utasaidia kupunguza idadi ya mahabusu magerezani, pia utasaidia Serikali
kupunguza gharama za kuwahudumia. Hatua hii itawapa fursa Majaji au Mahakimu kupata fursa ya kusikiliza mashauri mengine,’’ alisema Ngw’ilabuzu.
Aliongeza kuwa njia nyingine ya kupunguza mlundikano
huo ni vyema mtuhumiwa kupelekwa mahakamani wakati ushahidi ukiwa
umeshakamilika.
Kaimu Mkuu wa Mkoa huyo alisema siku za nyuma walikuwa
wanapokea malalamiko mengi kuhusu mashauri kukaa muda mrefu mahakamani au
kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama, lakini hivi sasa malalamiko hayo hayapo.
Hata hivyo, alisema kuwa changamoto iliyopo ni mashauri ya ardhi,
hivyo alishauri wanasheria wa Serikali, Mawakili na Mabaraza ya Ardhi
kushirikiana ili kuweza kutatua suala hilo. Pia alisema Serikali itaendelea
kushirikiana na Mahakama ili kuboresha miundombinu chakavu.
Aliwaomba wananchi kufika katika viwanja hivyo, ambapo maadhimisho hayo yameaanza leo tarehe 23
Januari, 2022 na yatamalizika tarehe 29 Januari, 2022, ili kupata elimu ya mambo mbalimbali kuhusu masuala ya kisheria. Kauli
mbiu ya maashimisho hayo ni ‘Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho kuelekea
Mahakama Mtandao’.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma alisema Kanda hiyo imeweza kusajili zaidi ya
mashauri 1,871 kati ya mashauri 2,225 yalisajiliwa kwa njia ya mtandao ambayo
ni sawa na asilimia 84. Aidha alisema kwa kipindi cha mwezi Desemba pekee jumla
ya mashauri 798 yalisikilizwa kwa njia ya ‘Video Conference’ katika ngazi zote
za Mahakama.
Alifafanua kuwa Kanda hiyo iliongoza kwa kusikiliza
mashauri mengi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mwezi
Desemba, ambapo ilisikiliza mashauri 6,352.
‘‘Kanda ya Dar es Salaam katika ngazi zote za Mahakama iliingia na jumla ya mashauri 13, 448 yaliyokuwa yamebakia kipindi cha mwaka
2020, huku jumla ya mashauri 39,031 yalifunguliwa na mashauri 40,146 yalisikilizwa na
kubakiwa na mashauri 12, 333. Kati ya mashauri yaliyobakia hadi kufikia mwaka
2021 ni asilimia 15,’’ alisema Jaji Mruma.
Jaji Mruma alisema ufanisi huo wa kazi umetokana na malengo ya kusikiliza mashauri ndani ya muda uliopangwa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni