Na Tiganya Vincent- Mahakama, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba
na Sheria imeridhika na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama
ya Tanzania unaoendelea mjini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa leo na
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Joseph Mhagama kwa niaba ya wajumbe wenzake
wakati wa ziara yao ya siku moja ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi
wa majengo matatu ya Mahakama.
Amesema kuwa wamefurahishwa na kazi
kubwa ambayo imekwishafanyika katika kusimamia na kuutekeleza mradi huo kwa
kiwango cha hali ya juu.
Dkt.Mhagama ameongeza kuwa kupitia
mradi huo ambao unatokana na fedha zilizotolewa na Serikali inaonyesha dhamira
ya dhati ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
alivyokusudia ili miguu ya Mihimili yote ya Serikali iwe pamoja mjini Dodoma.
Aidha, Kamati hiyo imeridhika na
hatua zinazochukuliwa za kuzingatia usalama wa wafanyakazi wanaotekeleza kazi
kwenye mradi na utoaji fursa kubwa za ajira nyingi kwa watumishi ambao ni raia
wa Kitanzania.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe
George Simbachawene amesema maendeleo ya ujenzi huo ni kielelezo na alama kuwa
Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na
Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha itatimiza ndoto za siku nyingi
za kutaka mihimili yote ya Serikali iwe katika makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma.
Amesema mihimili mingine kama vile
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali tayari imeshahamia Dodoma na
kukamilika kwa Jengo la Mahakama mihimili yote itakuwa pamoja Dodoma.
“Pongezi tunazitoa kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea
kuuwezesha muhimili wa Mahakama kifedha ili nao uweze kuhamia Dodoma …hatua
hiyo itaifanya Dodoma kuwa Capital City ya Tanzania kwa vitendo” amesisitiza.
Wakati huo huo, Mahakama ya Tanzania
inatarajia kuhamia mjini Dodoma mwaka huu baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa
wa ujenzi wa majengo ya Mahakama.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akitoa maelezo
ya maendeleo ya ujenzi wa majengo makubwa matatu ya Mahakama kwa Wajumbe wa
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyotembelea mradi huo kukagua
shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.
Amesema majengo hayo ambayo hadi
kukamilika yataragharimu kiasi cha shilingi bilioni 129.7 ambazo ni fedha
zinatokana na mapato ya ndani ya fedha za Serikali.
Prof. Gabriel amesema ujenzi huo
ambao utakuwa na jengo la Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu(
Supreme Courtupo katika hatua nzuri ambapo kazi kuwa zimekamilika kwa asilimia
kubwa.
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya
Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Mahakama katika miradi mbalimbali ukiwemo huo
kwa kutoa fedha kwa wakati jambo lililowafanya kasi ya ujenzi kuwa nzuri.
Kwa upande wa Msanifu Majengo kutoka
Kampuni ya Arqes Afrika ambaye ndiye wa michoro ya majengo hayo Rose Nestory
amesema kuwa majengo hayo yatakuwa na Sakafu tisa na kutakuwepo na ukumbi wenye
uwezo wa kuchukua watu 300 kwa wakati mmoja.
Amesema ujenzi wa majengo hayo
umezingatia sehemu ya kuendeshea shughuli za Mahakama, Ofisi za Utawala na
huduma nyingine.
Rose amesema katika eneo hilo
kutakuwepo na Migahawa, Uwanja wa kutua Ndege aina Helkopita , Uwanja wa
kuendeshea wiki na siku ya shughuli na kujenga
viwanja vya michezo na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya wadau wa
Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel(Mwenye kipaza sauti) akitoa maelezo leo kwa
Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati wa ziara yao ya
kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama akitoa maoni ya wenzake leo mjini
Dodoma kwa niaba ya wajumbe wenzake wakati wa ziara yao ya siku moja ya
kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama ya
Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel(Mwenye vazi la bluu) akiwa katika picha ya
pamoja leo na Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati
wa ziara yao ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa majengo ya Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania. Mwingine katika picha ni Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. George Simbachawene( wa saba kutoka kushoto kwa waliosimama).
Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge
ya Katiba na Sheria wakiwa katika picha ya pamoja leo mara baada ya ziara
yao kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi
wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania. Mwingine katika picha ni
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene( wa saba kutoka kushoto kwa
waliosimama).
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni