Na Faustine Kapama – Mahakama.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, tarehe 14 Februari, 2022 amefanya ziara ya siku
moja katika Mahakama ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga kukagua shughuli
mbalimbali za kimahakama na kuongea na watumishi.
Mhe. Chuma pia alipata nafasi ya kumtembelea Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Siriel Mchembe, kabla ya kukagua jengo la Mahakama lililopo Tanga Mjini, eneo linaloitwa Kange Kasera na baadaye kufanya mazungumzo na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor.
Akiwa katika Mahakama ya Wilaya
Handeni, Msajili Mkuu alipokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Mhe. Munga Sabuni pamoja na Afisa Utumishi wa Mahakama hiyo, Bw. Emmanuel Safari na kuongea na watumishi, ambapo alibaini changamoto kadhaa
na kutoa maelekezo mbalimbali.
Taarifa iliyowasilishwa kwake
ilianisha, pamoja na mambo mengine, changamoto kadhaa, ikiwemo Wananchi wa
Kwamsisi kutembea umbali mrefu wa kilomita 40 kutafuata huduma za Mahakama
Wilayani Handeni.
Maafisa hao walishauri kuwa masjala
ndogo ya Mahakama ya Wilaya Handeni ifunguliwe eneo la Mkata kwa lengo la kutatua
changamoto hiyo. Vilevile iliainishwa kuwa Mahakama ya Mwanzo Chanika iliyoko
Handeni Mjini inaupungufu wa Hakimu mmoja.
Aidha, viongozi hao walimweleza Mhe.
Chuma kuwa Mahakimu waliowengi, hususani Mahakama za Mwanzo wamekaa muda mrefu
zaidi ya miaka kumi na hivyo kupendekeza wahamishiwe vituo vingine.
Kadhalika, taarifa hiyo ilibainisha
kuwa Mahakama za Mwanzo Wilaya ya Handeni pamoja na Mahakama ya Wilaya
zinatengewa bajeti ndogo na kwamba mtandao wa intaneti unasusua na hivyo
kulazimu utendaji kazi, hususani usajili na uhuishaji wa taarifa za mashauri
kwenye mfumo wa JSD2 kuzorota.
Akijibu changamoto hizo, Msajili
Mkuu alieleza kuwa suala la mtandao linashughulikiwa na makao makuu na kwamba
juhudi zinafanyika ili kuingiza Mahakama zote nchini kwenye barabara ya mtandao
wa Serikali (eGovernment network). Alisema mara baada ya Mahakama zote nchini
kuingizwa kwenye mkongo wa taifa changamoto hiyo haitakuwepo tena.
Kuhusu suala la bajeti hususani katika
Mahakama za Mwanzo, Mhe. Chuma alisema, “Mhe. Jaji Mkuu ameshaelekeza kuwa
bajeti ya Mahakama za Mwanzo itazamwe upya.”
Akinukuu taarifa ya utendaji kazi wa
Mahakama ya mwaka 2021, Msajili Mkuu alisema kuwa Mahakama za Mwanzo zilisajili
asilimia 70 ya mashauri yote katika ngazi zote za Mahakama
na hivyo Mahakama za Mwanzo kuonekana kuwa na idadi kubwa ya mashauri.
Hata hivyo, Msajili Mkuu aliwahimiza
watumishi kuendelea kutumia TEHAMA katika kuratibu shughuli za Mahakama na
kutumia njia mbadala za mtandao wa intaneti katika kusajili na kuhuisha taarifa
za mashauri kwenye mfumo wa JSDS2,
Aidha, aliwataka kuendelea
kuwahudumia vizuri wananchi-Customer Care, hatua ambayo itasaidia kuongeza
imani ya Wananchi kwa Mahakama na kufanya kazi kwa umoja (team work) na
kudumisha upendo kati yao kwa sababu muda mrefu wanautumia kazini na hivyo
wanajumuika pamoja eneo la kazi kama familia moja.
Mhe. Chuma alihimiza kila mtumishi
kuwa mbunifu katika kutekeleza wajibu wake ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania
kuwa na mafanikio makubwa na kuzingatia maadili ya kazi kwa kuwa maadili
yanayohitajika mahakamani ni ya kiwango cha juu.
Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya,
Msajili Mkuu alimweleza Mhe. Mchembe kuwa yeye ni mdau mkubwa wa Mahakama na
kwamba ndiye mwenye wananchi, hivyo atumie majukwaa aliyonayo kuwaelimisha kuhusu uboreshaji unaofanyika na unaoendelea Mahakamani kwa lengo la
kurahisha huduma.
“Uboreshaji huu ni pamoja na
matumizi ya mifumo ya TEHAMA na namna bora wananchi wanavyoweza kuwasilisha
mrejesho kuhusu wanavyohudumiwa na Mahakama kwenye Kurugenzi ya Ukaguzi,
Maadili na Huduma za Mahakama,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya
alieleza kuwa ujio wa Msajili Mkuu ulimwezesha kufahamu uboreshaji mbalimbali uliofanyika
na unaoendelea Mahakamani tangu mwaka 2015. Aliomba Wakuu wa Wilaya, Watendaji
wa Vijiji na Kata kupewa elimu kuhusu uboreshaiji unaoendelea Mahakamani.
Wakati wa maongezi na Jaji Mfawidhi,
Msajili Mkuu alieleza changamoto alizobaini Handeni na katika ukaguzi wa jengo
la Mahakama Kange.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kulia) akizungumza na watendaji wengine wa Mahakama jijini Tanga alipofanya ziara ya siku moja tarehe 14 Februari, 2022 kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni