· Shahidi Kigoma asikilizwa kielektroniki
· Wadau waipongeza Mahakama Kanda ya Kigoma
Na Festo Sanga, Mahakama Kuu-Kigoma
Wadau wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Kigoma wameonesha kufurahishwa na Mahakama Kanda hiyo kwa kufanikiwa kumsikiliza shahidi wa Jamhuri kwa njia ya mtandao ‘video conference’ katika kikao cha kesi za Mauaji kinachoendeshwa chini ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Lameck Mlacha.
Shauri hilo la Mauaji namba 105/2014 linalomkabili Bw. Kinyota Kabwe lilisikilizwa katika kikao kilichoketi Mahakama Kuu Kigoma na kumuwezesha Shahidi wa Jamhuri, Bi Maines Nyaumba aliyeshindwa kufika mahakamani kutokea kuja kutoa ushahidi kwakuwa shahidi huyo alijifungua mtoto siku chache zilizopita hali iliyomsababisha kushindwa kusafiri.
Wakili wa serikali, Mkoa wa Kigoma, Bi Antia Julius aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kutunga kanuni hizo ambazo zinasaidia kumalizika kwa mashauri yenye mashahidi walio na changamoto za kufika Mahakamani kwa wakati.
“Tunaipongeza Mahakama ya Tanzania kwa Utekelezaji wa Vitendo kauli mbiu ya uboreshaji wa huduma zake kuelekea Mahakama Mtandao (e-Judiciary)” Aliongeza Bi Antia.
Usikilizaji wa Ushahidi kwa njia ya mtandao umeridhiwa kupitia Kanuni za Usikilizaji wa Mashauri kwa njia ya Mtandao (The judicature and application of Laws (Remote proceedings and Electronic recording) Rules) ulioanzishwa rasmi kwa Tangazo la Serikali namba 637 la tarehe 27 Agosti, 2021.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Mlacha alielekeza ushahidi wa shahidi huyo kuchukuliwa kwa njia za kieletroniki kwa kutumia kanuni ya sita (6) ambapo alimteua Bw. Prosper Mahalala, Afisa TEHAMA kuwa “Remote Proceedings Assistant”.
Bw. Mahalala aliongozana na Wakili Antia kwenda Kijiji cha Muzye wilayani Kasulu alipokuwa shahidi huyo ambapo ni zaidi ya kilomita 70 kutoka Mahakama Kuu Kigoma. Kwa kuzingatia matakwa ya kanuni ya 7 (f) ushahidi ulichukuliwa katika chumba cha jengo la Zahanati ya Kijiji cha Muzye ambapo kulikuwa na huduma ya mtandao na Umeme.
Katika kikao hicho kinachoendelea jumla ya mashauri ya mauaji saba (7) yanategemewa kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
Akifungua Mkutano wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mjini Arusha hivi karibuni, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwakumbusha Waheshimiwa Majaji hao kutosahau kutekeleza Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu 2022 inayosema ‘Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mtandao’ kwakuwa inachochea zaidi kasi ya maandalizi ya kuelekea kuwa na Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary.’
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni