Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu- Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha amekagua Miradi ya Ujenzi wa Mahakama tarajiwa za Wilaya ya Uvinza, Buhigwe na Kakonko inayoendelea kujengwa katika Kanda hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo aliyofanya tarehe 05 Februari, 2022, Mhe. Jaji Mlacha alimsisitiza mkandarasi wa Miradi hiyo ambaye ni ‘Lucas Construction CO LTD’ kuongeza kasi katika ujenzi kwa kuzingatia ubora.
“Kazi inakwenda vizuri japo mpo nyuma ya ratiba, tafadhali ongezeni kasi na kuzingatia viwango vya ubora” alisema Jaji Mlacha.
Miradi hiyo ya Ujenzi iliyoanza kujengwa rasmi tarehe 15 Oktoba, 2021 inatarajiwa kukamilika tarehe 30 Aprili mwaka huu.
Ujenzi wa Mahakama tatu (3) za Wilaya ya Buhigwe, Uvinza na Kakonko utawaondolea adha wananchi wa Wilaya hizo ambapo awali walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama Buhigwe (Kasulu), Uvinza (Kigoma) na Kakonko (Kibondo).
Aidha; majengo hayo yanayojengwa yatakuwa wezeshi katika miundombinu ya TEHAMA ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati mpya wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano (5) (2020/2021-2024/2025).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (kushoto) akisikiliza maelezo kuhusu ramani ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza kutoka kwa Fundi Mchundo Bw. Edwin Lucas alipotembelea Mradi huo. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu- Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka.
Mtendaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka akielezea jambo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha (katikati) na Wakandarasi wa 'Lucas Construction Co LTD' alipotembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni