Na Faustine Kapama – Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma ameainisha faida lukuki ambazo Mahakama ya Tanzania
imezipata kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika matumizi ya
teknolojia, ikiwemo kuharakisha utoaji wa haki na pia kuokoa zaidi ya shilingi billioni
2.750 za Kitanzania, kiasi ambacho kingetumika wakati wa kusikiliza mashauri
kwa njia ya kawaida.
Akizungumza leo tarehe 2 Februari,
2022 jijini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Sheria, kuashiria mwanzo wa
mwaka mpya wa shughuli za kimahakama nchini, Mhe. Prof. Juma amewasihi
watumishi wa Mahakama na wadau wote katika sekta ya Sheria kuendelea kuvuna
faida ya uwekezaji mkubwa katika teknolojia uliofanywa na Serikali katika
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Teknolojia.
“Uboreshaji unaoletwa kupitia teknolojia
unaorahisisha upatikanaji wa haki kwa kila mtu una faida ya kusogeza huduma za
utoaji haki na kuyafikia makundi yasiyojiweza, ambayo kwa kawaida huwa mbali na
huduma za kisheria na utoaji haki. Kwa njia hii, haki itapatikana kwa mizani ya
usawa. Baada ya kutungwa Sheria na Kanuni wezeshi, Mahakama ya Tanzania imeanza
safari ya kuelekea Mahakama Mtandao kwa lengo kuu la kuleta ufanisi, uwazi na
kuwapunguzia gharama wananchi na watumiaji wengine wa huduma za utoaji haki,”
amesema.
Jaji Mkuu amemweleza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi
kwenye maadhimisho hayo kuwa uamuzi wa Mahakama wa kutumia teknolojia na kuvuna
faida kutoka katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, ni kuhakikisha kuwa Tanzania inajenga
uchumi shindani na utoaji wa haki wenye viwango vinavyokidhi huo ushindani.
“Mahakama ya Tanzania haiwezi
kufumbia macho yale yanayoendelea katika jamii wala kubaki nyuma au kuendelea
kukumbatia mifumo ya kizamani ya uandishi wa mienendo mahakamani kwa mikono
wakati Akili Bandia ipo kuweza kufanya kazi hiyo kwa wepesi na bila gharama.
Mahakama ya Tanzania haiwezi kubaki katika zama za kianolojia iliyopitwa na
wakati katika mfumo wa utoaji haki,” amesema.
Jaji Mkuu amesema kuwa muda huu
kabla ya mwisho wa robo ya kwanza ya Karne hii ya 21 ndio wakati sahihi kwa
Mahakama ya Tanzania, kwa kushirikiana na Mihimili ya Serikali na Bunge, kuanzisha
mifumo ya kimahakama ya kidijitali kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya
kibiashara inayofanyika kidijitali.
Amesema uwekezaji uliofanywa na
Serikali ya Tanzania katika Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa umewezesha Mahakama
kuunganishwa vituo zaidi ya 157 kwenye Mkongo huo, ambapo kunganishwa huko
kumepanua matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ngazi
zote za Mahakama ya Tanzania na imewezesha upatikanaji wa haki kwa wakati.
“Kupitia Mkongo (huu wa Taifa),
Mahakama ya Tanzania imesogeza huduma (zake) karibu zaidi na wananchi. Aidha,
mifumo ya kielektroniki imeweka mazingira ambayo yamewezesha kubadilishana
taarifa kati ya Mahakama, taasisi na wadau katika mfumo mzima wa utoaji haki
nchini,” Mhe. Prof. Juma amesema.
Amemweleza Rais Samia pia kuwa moja
ya mafanikio makubwa ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli za utoaji haki ni kuwepo
kwa mfumo wa Kielekitroniki wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (JSDS2)
uliozinduliwa mwaka 2019 ambao umewezesha na kurahisisha usajili wa mashauri, Majaji
na Mahakimu Wafawidhi kuwapangia Majaji na Mahakimu mashauri ya kusikiliza na
utayarishaji wa kumbukumbu za mashauri kuanzia yanaposajiliwa hadi hatua ya
kutolewa hukumu au uamuzi.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kumekuwepo
na usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao unaowawezesha wadaawa na wadau walio
mbali na vituo vya Mahakama kusajili mashauri, nyaraka na viambatanishi wakati
wowote ule na kusambaza taarifa za mashauri kwa wahusika kupitia ujumbe mfupi.
Amesema kuwa mbali na kuunganishwa
na ule wa malipo ya Serikali (GePG) kuwezesha kulipa tozo, ada na faini kwa
njia ya mtandao, mfumo wa JSDS2 umerahisisha ukusanyaji wa takwimu za mashauri yaliyofunguliwa
katika ngazi yoyote ya Mahakama kwa njia za kawaida au mitandao pamoja na upakuaji
wa taarifa zote zinazohusika, ikiwemo mlundikano, mashauri yaliyotolewa uamuzi,
yanayoendelea na yale ambayo hayajapangwa kwa Majaji au Mahakimu.
Jaji Mkuu amesema pia kuwa uwekezaji
katika TEHAMA umeiwezesha Mahakama kuwa na mfumo wa Usajili, Usimamizi na
Utambuzi wa Mawakili ambao unawapambanua wenye leseni hai na kustahili kutoa
huduma za Uwakili. Amebainisha kuwa huduma nyingine ni upatikanaji wa uamuzi
unaotolewa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kwa kupitia mfumo wa TANZLII
na uwepo wa tovuti ya Mahakama yenye taarifa muhimu kwa wadau, wadaawa,
watumiaji wa huduma za Mahakama na wananchi wengine kwa ujumla.
Amesema kuwa Mahakama ya Tanzania
inatumia mfumo unaotekeleza majukumu mbalimbali yanayohusisha vikao kwa njia ya
video bila wahusika kulazimika kukutana ana kwa ana, teknolojia ambayo hutumika
kuendesha mashauri na kutoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi na wadau wengine.
“Mfumo huu umesimikwa katika vituo
vya Mahakama na pia katika baadhi ya Magereza. Kwa mwaka 2021 pekee, jumla ya
mashauri 17,979 yalisikilizwa kwa kutumia mfumo huu. Matumizi ya (mfumo huu)
yanakadiriwa kuokoa kiasi cha shilingi 2,750,092,736 za Kitanzania kwa mwaka
kwa upande wa Magereza, Mawakili, Mahakama na wadau wengine,” amesema.
Baadaye, Jaji Mkuu alikagua gwaride
maalum la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Polisi Tanzania kuashiria kuanza
rasmi kwa shughuli za kimahakama katika ngazi zote kwa mwaka 2022 kote nchini.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani wakifuatilia matukio mbalimbali katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman (kulia) akiwa pamoja na maafisa waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria leo tarehe 2 Februari, 2022 jinini Dodoma. Kutoka kulia kwa Mhe. Chande ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu, Mhe. Wilbert Martin Chuma na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni