Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaambia wadau wa haki nchini
kwamba katika zama za mapinduzi ya nne ya viwanda matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji haki hayaepukiki kwa kuwa suala
hilo ni mtambuka.
Akizungumza
katika kilele cha siku ya Sheria nchini, leo tarehe 2 Februari, 2022 katika
Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma, Mhe. Prof. Juma alisema, wadau wote
katika mnyororo wa haki wana jukumu la kuhakikisha TEHAMA inatawala mchakato
mzima wa utaoji haki katika hatua zote za uendeshaji wa mashauri na Mahakama
ikitembea yenyewe haitafika mbali.
“Safari
ya kuelekea Mahakama Mtandao haiwezi kamwe kufikiwa ikiwa wadau wa Mahakama
watabaki nyuma. Nichukue fursa hii kuwapongeza wadau wote wa Mahakama ambao
wameanza kuchukua hatua ya kuelekea katika matumizi ya TEHAMA”, alisema Jaji
Mkuu
Mhe.
Prof. Juma aliwaomba wadau wote wa Mahakama nchini kuchukua hatua za makusudi
sio tu kuunga mkono juhudi za Mahakama katika matumizi ya TEHAMA bali nao
watumie mfumo huo katika kutoa huduma zao.
Aidha,
Jaji Mkuu alikiri kuwa pamoja na jitihada za Mahakama za kutumia TEHAMA katika
utoaji haki, bado zipo sheria nyingi zinazokinzana na matumizi ya mfumo huo
katika utoaji haki nchini. Miongoni mwa sheria hizo ni sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai, Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai na Sheria ya Ushahidi
kwa kutaja chache.
“Nimeshamuomba
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasiliana na Uongozi wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ili kuangalia uwezekano wa kuzifanyia marekebisho sheria
hizo ziendane na hali ya sasa”, alisema Jaji Mkuu
Mhe.
Prof. Juma alisema, Mahakama imefanya marekebisho ya kanuni kadhaa za Jaji Mkuu
na kutunga kanuni mbili yaani Kanuni za ufunguaji wa mashauri kwa njia ya
mtandao “The Judicature and Application
of laws Electronic Failing Rules 2018”. Pamoja na Kanuni za usikilizaji wa
Mashauri kwa njia ya mtandao “The
Judicature and Application of laws Remote Proceedings and Electronic Recording
Rules 2021”.
Jaji
Mkuu aliongeza kuwa, Mahakama inaufanyia maboresho makubwa mfumo wake wa
Menejimenti ya Mashauri (JSDS II) ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Mfumo huu mpya utakuwa na hadhi ya “Advanced Case Management”. Mfumo huo
hautaruhusu ufunguaji wa mashauri kwa njia ya kawaida.
Mfumo
huo utakuwa na uwezo wa kutengeneza jalada la ki – elektroniki la shauri
“Electronic case file” na utawezesha ubadilishanaji wa majalada ya mashauri kwa
njia hiyo na kuweka saini ya ki – elektroniki kwenye kumbukumbu “Digital
Signature”, mfumo huo unatarajiwa kutumiwa hadi ngazi za Mahakama za Mwanzo.
“Mategemeo
yetu ni kuwa mafanikio ya mikakati yetu hiyo miwili itatufikisha katika hatua
ya kutotumia karatasi “Paperless Court” mpango ambao tumeuanza kwa majaribio
katika Mahakama ya Wilaya Kigamboni na kupata mafanikio na tumejifunza maeneo
ya kuboresha”, alisisitiza Jaji Mkuu.
Mhe.
Prof. Juma akadokeza mpango wa Mahakama wa kuanzisha kambi za mahema ya utoaji
haki “Justice Tents Camp” zitakazo tumika hasa katika maeneo yaliyopo mbali na
huduma za Mahakama na kwamba yatakuwa na
uratibu wa kuwekwa kwa ratiba maalum kutokana na mahitaji. Amesema kuwa
Mahakama hizo zitakuwa na Mahakimu na Majaji wasiokuwa na mipaka “Borderless
Judges and Magistartes” hii nikutambua kuwa kuna makundi ambayo sio rahisi
kufikiwa na huduma za Mahakama kutokana na jiografia yao na shughuli zao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni