Na Lydia Churi-Mahakama
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa kujikita katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ikiwemo kutafuta program maalum ya kutafsiri sheria kwa
lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuimarisha matumizi ya lugha hiyo katika kutoa
huduma za kimahakama.
Akizungumza
kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini
yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 2 Februari, 2022 katika viwanja vya Chinangali
jijini Dodoma, Rais Samia amesema program hiyo itakayotumiwa na Mahakama katika
kurahisisha shughuli za utoaji haki pia itatoa nafasi kwa lugha ya Kiswahili
kupata tafsiri na unukuzi kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine za
kigeni.
Rais
Samia ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema Serikali inaunga
mkono kikamilifu jitihada zinazofanywa na Mhimili wa Mahakama katika kuwekeza
kwenye Teknolojia na kuwataka viongozi wa Mahakama kuongeza kasi kwenye
matumizi hayo ili kurahisisha shughuli za utoaji haki.
Alisema
Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye matumizi ya TEHAMA hususani katika
kutengeneza mifumo yake mbalimbali ya kurahisisha kazi ya utoaji haki ukiwemo ule
wa kuhifadhi maamuzi mbalimbali yanayotolewa na Majaji (Tanzlii) na kuongeza
kuwa mfumo huu utasaidia kuongeza uwazi wa uamuzi wa Mahakama unaotolewa kwenye
mashauri mbalimbali.
Aidha,
Rais Samia ametoa wito kwa Sekta ya Sheria nchini kuwatayarisha wahitimu na
kuwaongezea ujuzi wanasheria walioko makazini ili waendane na wimbi la ukuaji
wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
“Dunia
iko kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda yanayoongozwa na matumizi ya TEHAMA,
hivyo uchumi wa dunia pamoja na shughuli mbalimbali zikiwemo za utoaji haki
zinaendeshwa kwa kutumia Teknolojia hiyo”, alisema Rais Samia.
Amezitaka
wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Wizara ya
Elimu, Sayansi na Vyuo Vikuu vyote kuhakikisha wanafunzi kuanzia shule za
msingi hadi vyuo vikuu wanapatiwa ujuzi ili kuwaandaa kufanya kazi zinazohitaji
ujuzi unaolingana na matakwa ya mabadiliko ya Teknolojia.
Alisema
wakati tulionao sasa unahitaji mabadiliko makubwa ya kifikra na kuzalisha nguvu
kazi yenye ujuzi linganifu na mabadiliko ya teknolojia duniani. “Tanzania
haiwezi kubaki nje ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambayo yanaendelea
kubadilisha mizani ya ushindani katika shughuli zote za kibinadamu zikiwemo za
uwekezaji na mazingira ya biashara”, alisema.
Rais
Samia pia amewataka Majaji na Mahakimu kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia
Sheria na Katiba ya nchi na kutenda haki kwa watu wote bila kuangalia hali ya
mtu kiuchumi na kijamii.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameziomba Wizara za
Nishati na ile ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoa huduma za
uhakika ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania pamoja na sekta ya sheria kwa
ujumla kutumia Tehama katika kurahisisha shughuli za utoaji haki.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Taasisi waliohudhuria kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na siku ya Sheria nchini leo katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma. Wa tatu kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson na wa tatu kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Waheshimiwa Majaji Wastaafu wa Mahakama ya Rufani pamoja na Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Waheshimiwa Mawaziri waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni