Na. Francisca Swai-Mahakama, Musoma.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya jana tarehe 18
Machi, 2022 alikagua, ikiwemo maendeleo ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Butiama
na kumsisitizia Mhandisi, Bw. Bakari Abdallah wa kampuni ya United Builders kukamilisha
mradi huko kwa wakati na viwango vinavyokubalika.
Akiwa katika ziara ya
siku tano kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama ndani ya Kanda hiyo, Mhe.
Mtulya alisema ujenzi imara wa majengo utawezesha miundombinu hiyo ya Mahakama kutumika
kwa muda mrefu.
Alionya kukimbizana na
muda kukamilisha kazi kwa muda mfupi kunaweza kusababisha baadaye kujitokeza mapungufu
makubwa kwenye majengo hayo. Mradi wa ujenzi wa Mahakama hiyo unatarajiwa kukamilika
tarehe 12 Aprili, 2022.
Katika ziara hiyo, Jaji
Mfawidhi huyo pia ametembelea Mahakama ya Mwanzo Nansimo iliyojengwa wakati wa
mkoloni mwaka 1928 ambayo ilifungwa mwaka 2014 kutokana na fujo za wananchi
dhidi ya Mahakama.
Mhe. Mtulya alikutana
na Mtendaji wa Kijiji cha Nansimo, Bw. Bwire Manumbu ambaye ameonesha nia ya
kutoa chumba cha mikutano katika Ofisi ya Tarafa ili kiweze kutumika kwa
shughuli za Mahakama, kwani wananchi wa eneo hilo lenye Kata sita wanalazimika
kufuata huduma za kimahakama umbali wa Kilometa 30 katika Mahakama ya Mwanzo
Kenkombyo, hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi za wananchi hao.
Jaji Mfawidhi huyo amewaelekeza
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi na Mtendaji wa
Mahakama katika Kanda hiyo, Bw. Festo Chonya kuhakikisha hadi ifikapo tarehe 25
April, 2022, Mahakama hiyo ianze kutembelewa.
Wakati huo huo alimtaka
Mtendaji wa Kanda kuendelea na ukarabati wa jengo lililopo hadi hapo Mahakama
hiyo itakapojengwa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, kwani iko katika orodha
ya majengo yatakayojengwa ili kuwapunguzia wananchi adha ya kupoteza muda
mwingi kufuata huduma za kimahakama.
Pamoja na ukaguzi wa
ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Butiama, Jaji Mfawidhi huyo alikagua Mahakama za
Mwanzo Bunda Mjini, Kukirango, Kabasa, Nansimo, Kenkombyo na Mahakama ya Wilaya
Bunda. Katika ziara hiyo, Mhe. Mtulya
anatarajiwa kukagua Mahakama zote zilizoko Kanda ya Musoma ili kuona mazingira
halisi ya utendaji kazi.
Akiwa katika Mahakama
hizo alizotembelea, Jaji Mfawidhi huyo alipokea kutoka kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi
taarifa mbalimbali za utendaji kazi zinazoonesha utendaji kazi wa kuridhisha, ikiwemo
umalizaji wa mashauri kwa wakati, nidhamu kwa watumishi, utunzaji wa mazingira,
jitihada za kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani, ushirikiano na wadau
pamoja na ukarabati mdogo mdogo wa majengo ya Mahakama.
Aidha, Mhe. Mtulya katika
ziara yake alipata nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Bunda na kukutana
na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bw. Salum Mtelela na kushukuru kwa ushirikiano
mkubwa uliopo na Mahakama ya Wilaya Bunda.
Katika ziara hiyo,
changamoto mbalimbali ziliibuliwa ikiwemo uhaba wa rasilimali watu unaopelekea
watumishi kufanya kazi zaidi ya zile walizoajiriwa, malimbikizo ya mishahara, mlundikano
wa majalada ya miaka ya zamani, uchakavu wa baadhi ya majengo ya Mahakama,
ukosefu wa huduma za maji na umeme katika badhi ya Mahakama pamoja na ufinyu wa
bajeti.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa
eneo la mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Butiama.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kushoto) akisisiza
jambo wakati wa kikao kifupi na viongozi wa Mahakama pamoja na msimamizi wa ujenzi
wa Mahakama ya Wilaya Butiama kutoka kampuni ya United Builders baada ya kukagua
mradi huo.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto)
akiteta jambo na viongozi wa Mahakama kutoka Kanda, Mahakama ya Wilaya Bunda na
watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Kabasa baada ya ukaguzi wa Mahakama hiyo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Mwanzo Kabasa, Mhe. Isaya Kitula (aliyesimama) akisoma taarifa
ya utendaji kazi mbela ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.
Hakimu Mkazi Mfawidhi
Mahakama ya Mwanzo Bunda Mjini, Mhe. Stella Shayo akisoma taarifa ya utendaji
kazi wa Mahakama hiyo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya a(wa pili
kushoto) kiteta jambo na viongozi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma pamoja na Mahakama
ya Wilaya Bunda kuhusu ukarabati wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nansimo
iliyofungwa mwaka 2014.
Mtendaji wa Kijiji cha
Nansimo Bw. Bwire Manumbu Bwire (wa tatu kushoto) akielezea jambo kuhusu chumba
anachopendekeza kianze kutumika kwa ajili ya Mahakama ya Mwanzo Nansimo hadi
hapo Mahakama hiyo itakapojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akikabidhi
vitendea kazi kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kenkombyo Mhe.
Victoria Gambamala wakati wa ukaguzi wa mahakama hiyo ambapo pia alimpongeza kwa
utendaji kazi mzuri wa kumaliza mashauri mengi kwa wakati.
Hakimu Mkazi Mfawidhi
Mahakama ya Wilaya Bunda, Mhe. Mulokozi Kamuntu (aliyesimama) akiwasilisha
taarifa ya utendaji kazi wa kituo hicho kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni