Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma amewataka
maafisa upelelezi ndani ya Kanda hiyo kukamilisha upelelezi kwa haraka ili mashauri
ya jinai yaliyopo mahakamani yamalizike kwa wakati.
Mhe. Matuma alitoa wito
huo alipokuwa akizungumza na maafisa upelelezi kutoka Mikoa ya Shinyanga na
Simiyu tarehe hivi karibuni.
Jaji Mfawidhi huyo
aliwahimiza maafisa hao kutoka Jeshi la Polisi kuchuja vielelezo na ushahidi
unaowasilishwa mahakamani ili kuondoa mashaka yanayoweza kujitokeza wakati wa usikilizaji
wa mashauri hayo.
“Wapo baadhi ya
wapelelezi huchelewesha upelelezi kwa makusudi na kusababisha shauri kukaa mahakamani
kwa muda mrefu hata zaidi ya miaka mitatu. Wapelelezi wa namna hii
hatutawavumilia katika Kanda yetu ya Shinyanga,” alionya Mhe. Matuma.
Aidha, Jaji Mfawidhi
huyo aliwasisitiza maafisa hao wa upelelezi na Mahakimu wote wa Kanda ya
Shinyanga kuhakikisha watuhumiwa ambao wanadhaminika na waliotimiza masharti ya
dhamana wanapewe dhamana ili kuondoa mlundikano wa mahabusu Magereza.
“Wapo baadhi ya askari
wapelelezi kwa kushirikiana na baadhi ya Mahakimu wamekuwa wakizuia dhamana kwa
watuhumiwa ambao wanastahili kupewa dhamana. Ni heri kuwaachilia huru watu mia
moja wenye hatia kuliko kumtia hatiani mtu mmoja asiye na hatia,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mhe.
Matuma amewapongeza maafisa wa TAKUKURU kwa kufanfanya kazi zao kwa umakini na
kwa weledi. “Niwapongeze TAKUKURU, nimefanya kazi nao muda mrefu wanawasilisha ushahidi
na vielelezo vilivyojitosheleza, niwaombe muendelee na kazi hiyo nzuri,” aliongeza.
Kikao hicho ni
muendelezo wa vikao kazi kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Shinyanga pamoja na wadau wanaofanya kazi kwa karibu na Mahakama katika kutatua
changamoto mbalimbali ili kushirikiana pamoja katika kutekeleza Mpango Mkakati
wa Mahakama ya Tanzania 2020/21 – 2024/25.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma (kushoto)
akisisitiza jambo wakati wa kikao maalum na maafisa upelelezi na na Magereza
Kanda ya Shinyanga (hawapo katika picha). Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kanda
ya Shinyanga Bi. Mavis Miti.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mhe Mary Mrio (aliyesimama) akisisitiza jambo
wakati wa kikao na maafisa upelelezi na magereza Kanda ya Shinyanga.
Sehemu ya Maafisa wa TAKUKURU kutoka Wilaya zilizopo Kanda ya Shinyanga wakimsikiliza Jaji Mafwidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athumani Matuma (hayupo katika picha) wakati wa kikao kazi maalum kilichofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga.
Mrakibu wa Polisi Suleman Juma kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Shinyanga akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Mrakibu wa Magereza SP D. Kapesa kutoka Magereza Simiyu akichangia jambo wakati wa kikao na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mh. Athuman Matuma (hayupo katika picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni