Na. Francisca Swai – Mahakama, Musoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewaasa watumishi mahakamani
kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama ili kuepusha kuvamiwa na wananchi.
Akiwa katika siku ya
pili ya ziara yake ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za kiutendaji za kimahakama,
Mhe. Mtulya amesisitiza utambuzi wa mipaka yote ya Mahakama katika
Kanda hiyo na kuwahimiza viongozi wa maeneo husika kuweka alama stahiki.
Amemwelekeza Mtendaji
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya kutayarisha mpango maalumu
wa kuweka alama tambuzi za kudumu katika maeneo yote ya Mahakama licha ya
baadhi ya maeneo kuwa na mipaka ya miti pamoja na katani.
Aidha, Jaji Mfawidhi
huyo amewasisitiza Mahakimu na watumishi wote kufanya kazi kwa bidii, hususani kuyapa
kipaumbele mashauri ya ndoa, talaka na mirathi kwa vile yana athari za moja kwa
moja katika familia.
Katika ziara hiyo, Mhe.
Jaji Mtulya alitembelea na kujionea Mahakama mbalimbali ikiwemo Mahakama ya
Mwanzo Mcharo na Mugeta zinazofanya kazi katika Ofisi za Tarafa katika maeneo
yao na Mahakama ya Mwanzo Mugumu inayotumia jengo la Halmashauri ya Wilaya ya
Serengeti.
Alibainisha kuwa Mahakama
zote hizo tayari zina maeneo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama mpya za
kisasa kupitia mradi wa Benki ya Dunia.
Kadhalika, Mhe. Mtulya
alipata nafasi ya kutembelea Mahakama ya Mwanzo Robada ambayo ni ya kisasa
iliyopo katika eneo la Hifadhi ya Mbuga ya Serengeti katika kijiji cha Robanda,
umbali wa Kilometa 45 kutoka Serengeti mjini (Mugumu).
Jaji Mfawidhi huyo amempongeza
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Akinyi Mlowa kwa kufanya kazi kwa
bidii licha ya kuwa katika mazingira hatarishi yanayozungukwa na wanyama wakali
wa aina mbalimbali.
Akitoa taarifa ya hali
ya usalama mbele ya Mhe. Mtulya, Hakimu Mlowa
alisema sehemu ambayo Mahakama yake imejengwa inazungukwa na milima na
mapori ambayo ni makazi ya wanyama kama vile tembo, simba, nyoka, nyani,
tumbili na wengine.
Hakimu huyo alielezea
hatari inayomkabili katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo uvamizi wa
wanyama hao mahakamani hapo, ambapo siku za hivi karibuni kumekuwepo na uvamizi wa simba. Hata hivyo, Mhe. Mlowa alimweleza Jaji Mfawidhi
huyo kuwa Mlinzi wa kibarua, Bw. Omary Marongori amekuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na
wanyama hao.
Naye Mtendaji wa Kijiji
hicho, Bw. Jumanne Kiriba alisema hivi karibuni uvamizi wa Simba wanaoshambulia
mifugo ya wananchi umeongezeka na kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa
Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) walifanikiwa kuwakamata watatu ingawa tishio
la usalama bado ni kubwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kulia) akikabidhi
vitendea kazi kwa watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Mugumu Mjini.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Serengeti, Mhe. Jacob Ndira (aliyesimama) akipokea maelekezo kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya alipotembelea Mahakama hiyo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Mwanzo Mcharo, Mhe. Godfrey Simbeye (aliyesimama) akisoma
taarifa ya utendaji kazi mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa tatu kushoto) akikagua
eneo linalohifadhi majala ya miaka ya nyuma 1990, 1980 na kadhalika yaliyopo
Mahakama ya Mwanzo Natta. Amemwelekeza Naibu Msajili wa Mahama Kuu, Kanda ya
Musoma, Mhe. Frank Moshi kufuatilia utaratibu wa namna ya kuyaondoa majalada
hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kulia) akiongea na
watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Mugumu Mjini akiwemo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Mhe. Felix Ginene pamoja (aliyavaa t-shirt nyekundu).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni