Na Ahmed Mbilinyi- Mahakama, Bukoba
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Bukoba, Mhe. Angaza Mwipopo hivi karibuni alizindua Kamati ya Mawakili ya Mkoa
wa Kagera na kuhimiza wajumbe kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na
maadili ya hali ya juu.
Uzinduzi wa Kamati hiyo inayojulikana kwa Kiingereza
kama ‘Kagera Regional Advocate Committee’ ulifanyika ofisini kwa Mhe. Mwipopo
katika jengo la mahakama Kuu mjini Bukoba.
Jaji huyo aliwasisitiza wajumbe wa Kamati hiyo kufanyakazi
kwa weledi na kutenda haki bila upendeleo kwa kuzingatia moja ya majukumu ya kamati
ni kupokea malalamiko ya wateja yanayohusu huduma za uwakili wanazopokea kutoka
kwa Mawakili.
Mhe. Mwipopo aliongeza kuwa kazi ya Wakili sio tu kufanya
biashara bali pia ni huduma muhimu ambayo inatakiwa kutolewa kwa maadili ya hali
ya juu na weledi mkubwa.
“Fanyeni majukumu
yenu kwa mujibu wa sheria, msiende nje ya mipaka yenu,” alisema Jaji Mwipopo.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Msajili
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba, Mhe. Odira Amworo, ambaye ni Mwenyekiti na Wakili
wa Serikari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikari, Mhe. Nestory
Nchimani, ambaye ndiye Katibu wa kamati.
Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Wakili wa Serikari
Mwandamizi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mhe. Juma Masanja na Mwenyekiti wa Chama
cha wanasheria Mkoa wa Kagera, Mhe. Peter Matete.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni