Na. Francisca Swai - Musoma
Mahakama ya Tanzania,
Kanda ya Musoma, inaendesha zoezi la kuboresha majengo ya Mahakama za Mwanzo kupitia
fedha za matumizi ya kawaida ili kuimarisha miundombinu hiyo na kuweka
mazingira bora ya kufanyia kazi yanayochochea usikilizaji wa mashauri kwa urahisi
na haraka kwa wananachi.
Hayo yalibainika katika
siku ya tatu ya ziara anayofanya Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, kukagua
shughuli mbalimbali za kimahakama na kujionea ukarabati wa majengo hayo
unaoendelea.
Akiwa katika Mahakama ya
Mwanzo Ngoreme, Mhe. Mtulya amempongeza Mtendaji
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya kwa usimamizi mzuri wa rasilimali
fedha ambao umeleta matokeo chanya na mabadiliko makubwa katika miundombinu na mazingira ya Mahakama
kwa ujumla.
Mahakama ya Mwanzo Ngoreme
iliyopo wilayani Serengeti ambayo ilikuwa katika hali mbaya ni moja kati ya Mahakama
tatu zilizokuwa katika mpango wa uboreshaji wa miundombinu kupitia fedha za
matumizi ya kawaida (OC) kwa mwaka 2021/2022 uliowekwa na uongozi wa Kanda ya Musoma.
Baadhi ya Mahakama zilizofanyiwa
ukarabati mkubwa kupitia fedha za hizo ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Bunda Mjini,
Mahakama ya Mwanzo Kukirango na Mahakama ya Mwanzo Ngoreme. Pia zipo Mahakama zilizofanyiwa
uboreshaji mdogo mdogo, ikiwemo ili kuimarisha miundombinu yake.
Mahakama hizo ni Mahakama
ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Mwanzo Kabasa, Mahakama ya Mwanzo Kinesi pamoja
na Mahakama ya Mwanzo Nyaburongo.
Aidha, Jaji Mfawidhi
huyo amewapongeza Mahakimu na watumishi kwa utendaji kazi mzuri unaoridhisha na
kuwasisitiza Mahakimu kusikiliza mashauri kwa kufuata taratibu na kuyamaliza kwa
wakati.
Amemwelekeza Naibu Msajili
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi kuwaandikia barua za pongezi
Mahakimu wote wanaofanya kazi vizuri katika eneo hilo, huku akielekeza
kuandikiwa barua Mahakimu wote wanaobaki nyuma ili waeleze changamoto walizonazo
ziweze kutatuliwa kwa pamoja.
Akipokea pongezi hizo zilizotolewa,
Mtendaji huyo wa Mahakama Kuu wa Kanda aliwashukuru na kuwapongeza maafisa Tawala
na Utumishi wa maeneo husika kwa usimamizi wa karibu wa uboreshaji huo.
Alitolea mfano wa Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ngoreme, Mhe. Peter Malima na Mlinzi wa Mahakama
hiyo, Bw. Chacha Nsaho ambao wamekuwa msaada mkubwa na waaminifu katika kusimamia
mafundi pamoja na vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo.
Alimhakikishia Jaji
Mfawidhi kuwa ukarabati wa majengo ya Mahakama katika Kanda yake utaendelea kadri
upatikanaji wa fedha unavyoruhusu.
Muonekano wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Ngoreme ambapo
ujenzi unaendelea kwa kutumia fedha za matumizi ya kawaida (OC).
Muonekano wa zamani wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Ngoreme
lililokuwa na changamoto ya paa na uchakavu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma,
Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akikabidhi vitendea kazi kwa HakimuMkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Mwanzo Ngoreme, Mhe. Adam Malima (kushoto) na Mlinzi wa Mahakama
hiyo, Bw. Chacha Nsaho (kulia). Watumishi hawa walipongezwa kwa uaminifu katika
usimamizi wa ujenzi unaoendelea wa Mahakama ya Mwanzo Ngoreme.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya ( kulia) akiongea na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo
Nyamwaga akiwemo Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Adeline Kashushura (wa tatu kulia)
na Msaidizi wa Ofisi, Bw. Jasper Mrema (mwenye shati jeupe). Amewapongeza kwa utunzaji
mzuri wa mazingira na kulinda mipaka ya eneo la Mahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kenyana, Mhe. Ileon Ponella (kushoto) na Diwani wa Kata ya Ring’wani iliyopo Mahakama hiyo, Mhe. Hellena Chacha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma,
Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akimwelekeza jambo fundi msimamizi wa ujenzi wa
Mahakama ya Mwanzo Ngoreme, Bw. Alex Kicha (kulia) wakati wa ukaguzi wa ujenzi unaoendelea
mahakamani hapo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akiteta na viongozi wa Kanda pamoja na Mahakama wa Wilaya ya Tarime alipotembelea Mahakama ya Mwanzo Nyamongo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni