Na Innocent Kansha - Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha wanazuoni wa
taaluma ya Sheria kuchangamkia fursa za tasnia hiyo zinazojitokeza nje ya
mipaka ya nchi ili kukuza ushindani na soko la taaluma hiyo hasa kwenye nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza
na Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo na Ujumbe
wake walipomtemebelea ofisini kwake kwa ajili ya kumsalimu na kujitambulisha
Jijini Dar es salaam, leo tarehe 31 Machi, 2022, Prof. Juma amesema Tanzania
kama nchi imekuwa mstari wa nyuma kuchangamkia fursa zinazojitokeza nje ya
mipaka kwenye tasnia ya sheria.
“Nawasii
wanasheria wa Tanzania kuzitafuta na kuziona hizi fursa za kibiashara zinazoongezeka
kila kukicha na kuzitendea haki, nadhani ni wakati muafaka wa kuondokana na uwakili
wa karne ya 21 wa kuajiriwa, kuwa na ofisi ya uwakili kukutana na mteja ofisini
ili kupata kazi ya kipato,” alisema Jaji Mkuu.
Mhe.
Prof. Juma amesema taaluma ya sheria inabadilika kulingana na kasi ya ukuaji wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo ushindani ni mkubwa na kuna
nafasi za kutumia taaluma ya sheria nje ya mipaka kuliko ndani ya mipaka.
“Jumuiya
ya Afrika Mashariki inakuwa, kuna mwanachama mpya wa Jumuiya mwenye watu
takribani milioni 90. Je wanazuoni wa sheria watatumiaje nafasi hiyo kujenga
daraja la kibiashara ili kuendeleza taalumu zao? Takribani asilimia 80 ya
mawakili wanaohitimu kila mwaka nchini hawapati ajira za kudumu,” amesema.
Jaji
Mkuu ameueleza Ujumbe huo kuwa yupo tayari kupokea changamoto mpya za kukuza
ushindani wa kitaaluma na si kwa Tanzania pekee bali hata nje ya mipaka ili
kutengeneza misingi itayoifanya taaluma hiyo kukua na kuchangia kwenye pato la
taifa kwa ujumla.
Amebainisha eneo lingine la kuimarishwa kwa tasnia ili kuondoa kikwazo cha kibiashara ni lugha ambayo bado ni kikwazo, hivyo jumuiya inapaswa kuja na agenda ya kutatua changamoto hiyo ya mawasiliano hasa katika kipindi hiki cha karne ya 21 inayotawaliwa na mapinduzi ya nne ya viwanda.
Mhe.
Prof. Juma amesema kuwa Kiswahili hakijawezeshwa vya kutosha kiteknolojia ili
kiweze kushindana na lugha zingine za kimataifa mfano Kiingereza.
Kwa
upande wake Rais wa chama hicho Mhe. Oundo, alisema madhumuni ya uanzishwaji wa
Chama cha wanasheria Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kujenga na kuendeleza
taaluma ya sheria, kukuza utawala bora na utawala wa sheria na kuimarisha
ushirikiano miongoni mwa wanajumuiya.
Pia,
Rais huyo alitanabaisha kuwa ujio wake nchini unalenga kuhimiza na kuongeza
hamasa kwa wananchama wa Chama hicho Kikanda, kujaribu kuangaza fursa muhimu za
kibiashara kwa wanasheria na kuomba ushauri wa namna ya kukuza tasnia ya sheria
ndani ya Jumuiya.
“Kimsingi tumekubaliana na Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Juma kwamba, wanachama wetu waanze sasa kuwa na mtazamo
chanya wa kutoa huduma za kibiashara na kuangaza mambo katika wigo mpana wa
kuendeleza Jumuiya na sio kutoa huduma kwa kuegemea sera za kitaifa kwa
kuangalia fursa za nje ya mipaka”, alisema Rais huyo
Aidha,
Rais wa Chama hicho akatumia nafasi hiyo kuualika Uongozi wa Mahakama ya
Tanzania ili kutoa ushirikiana katika maandalizi ya mkutanao Mkuu wa mwaka wa
Chama hicho utakaofanyika mwezi Novemba, 2022 Jijini Arusha na katika mkutano
huo kutakuwa na uchaguzi wa kumpata Rais wa Chama hicho ambaye anatarajiwa
kutoka nchini Tanzania.
Rais
Oundo akamdokeza Jaji Mkuu kuwa Chama chicho kinatarajia tarehe 1 Aprili, 2022 kuendesha
mafunzo maalumu ya namna ya kushiriki kikamilifu fursa ya ujenzi wa bomba la
Mafuta litakaloanzia Ohima Uganda hadi Tanga Tanzania kwa wanachama wa Chama
cha Wanasheria Tanganyika.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Rais wa Chama cha Wanasheria
Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo na Ujumbe wake (hawapo pichani) mara walipomtemebelea
ofisini kwake kwa ajili ya kumsalimu na kujitambulisha Jijini Dar es salaam,
leo tarehe 31 Machi, 2022.
Rais wa Chama cha
Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kulia) akitia saini
kitabu cha wageni Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma alipowasili kufanya mazungumzo naye, wengine ni Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), Mhe. Prof. Edward Hosea (wa kwanza Kushoto) na Naibu
Mhasibu wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Bi. Hafsa Sasya (wa kwanza
kulia)
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto) akikabidhiwa zawadi ya kitabu
kilichoandikwa na Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki na Rais wa Chama
chicho Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kulia)
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto) akimkabidhi zawadi ya kitabu cha
Mpango Mkakati awamu ya pili wa mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 pamoja na machapisho
mengine ya Mahakama kwa Rais wa Chama chicho Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza
kulia)
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa
Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kushoto) Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mhe. Prof. Edward Hosea (wa kwanza
Kulia) mara walipomtembelea Ofisini kwake.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa
Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Mhe. Bernard Oundo (wa kwanza kushoto) Naibu
Mhasibu wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki Bi. Hafsa Sasya (wa kwanza
kulia) mara walipomtembelea Ofisini
kwake.
Picha na Innocent Kansha
- Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni