Alhamisi, 31 Machi 2022

JAJI MFAWIDHI MBEYA AHIMIZA UADILIFU, NIDHAMU, USHIRIKIANO KWA WATUMISHI

 Na Mohamed Kimungu-Mahakama, Songwe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim amewahimiza watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, nidhamu, weledi na ushirikiano wanapotekelea majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.

Mhe. Ebrahim alitoa wito huo jana tarehe 30 Machi, 2022 baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili aliyoifanya kuanzia tarehe 29 Machi, 2022 ambapo alitembelea  Mahakama ya Wilaya Ileje na Mahakama ya Wilaya Momba Mkoa wa Songwe na kuzungumza na watumishi.

Jaji Mfawidhi huyo ameupongeza Mkoa huo kwa kutokuwa na malalamiko katika utendaji wa kazi na katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Amewashauri watumishi wa kada zingine kujifunza TEHEMA kwa kuwa ndio uelekeo wa Mahakama kwa sasa kama inavyosisitizwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamisi Juma.

Katika ziara hiyo, Mhe. Ebrahim alitembelea pia mradi wa wa ujenzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe na kumuelekeza mkandarasi kumaliza mradi huo ifikapo tarehe 31 Mei, 2022 kama ilivyopangwa.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo amemtembelea Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe Ana Gidarya na kupongeza uongozi wake kwa umoja na ushirikiano unaotoa kwa Mahakama katika Wilaya hiyo. Kadhalika, Mhe. Ebrahim alitembelea Gereza la Wilaya ya Mbozi ambapo ameahidi kufanyia kazi changamoto kadhaa alizoziona.

Vile vile, Jaji Mfawidhi huyo amewapongeza Waendesha Mashtaka na  Ofisi ya Upelelezi katika Mkoa wa Songwe kwa kazi nzuri wanayofanya, hususani katika kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim (wa pili kulia) akipokea maelezo kutoka kwa mtendaji wa Mahakama, Bw. Sostenes Mayoka (wa pili kushoto) alipotembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim (wa kwanza kushoto) akikagua vizimba ndani ya jengo la Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim (wa pili kulia) akitambulishwa kwa watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Timothy lyon Hakimu (wa tatu kulia).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim (wa pili kulia mstari wa mbele) akitambulishwa kwa watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Ileje na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Desdery Magezi (wa tatu kulia mstari wa mbele).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ileje. Mhe Ana Gidarya (wa tatu kulia) na watumishi wengine).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni