- Yakiri Mradi huo kuendana na thamani ya fedha
- Viongozi IJA na Mahakama wapongezwa kwa usimamizi thabiti wa miradi ya ujenzi
Na Mary Gwera, Mahakama-Lushoto&Same
Ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria leo tarehe 16 Machi, 2022 imetembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Bweni (Hostel) la Wavulana unaojengwa katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto huku ikipongeza Uongozi wa Chuo hicho pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa kusimamia vyema Mradi huo unaoendana na thamani ya fedha.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa jengo hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Emmanuel Mwakasaka amesema kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa wameridhishwa na ubora wa jengo hilo ambalo mpaka kukamilika kwake linatarajiwa kugharimu kiasi cha fedha za kitanzania bilioni 2.6.
“Tumekagua hosteli hiyo tumeona, kwa muonekano na ubora kwakweli jengo linaendana na thamani ya fedha, kwa hili napenda kuupongeza Uongozi wa Chuo na Mahakama kwa kuendelea kusimamia vyema miradi ya ujenzi ambayo mingi inaonekana kuwa na viwango vinavyotakiwa,” alisema Mhe. Mwakasaka.
Aidha, Mhe. Mwakasaka ametoa rai kwa Uongozi wa Chuo cha IJA kuwa na mipango endelevu ambayo itawawezesha kujengo hosteli za kutosha ili wanafunzi wanaosoma katika Chuo hicho wote waweze kuishi ndani ya Chuo na si uraiani.
“Si salama sana wanafunzi kukaa mitaani, hivyo niwaombe kuwa na mipango endelevu itakayowezesha kuongeza idadi ya mabweni ‘hostels’ ili wanafunzi wote waweze kukaa ndani ya chuo,” aliongeza Mhe. Mwakasaka.
Akiwasilisha taarifa ya Miradi ya Ujenzi wa Daharia hiyo pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Same na Mwanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa ujenzi wa bweni hilo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha fedha za kitanzania bilioni 2.6.
“Mhe. Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati hii, Mradi huu wa ujenzi wa (hostel) utagharimu bilioni 2.6 na pindi utakapokamilika unatarajiwa kubeba wanafunzi 320,” alieleza Prof. Ole Gabriel.
Aidha; Mtendaji Mkuu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa rasilimali fedha za kuwezesha miradi mbalimbali na kuongeza kuwa pindi Bweni hilo litakapokamilika litakuwa ni mkombozi mkubwa kwa Wanafunzi wa Chuo hicho.
Naye Kaimu Mkuu cha Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)-Lushoto, Bw. Goodluck Chuwa ametoa shukrani kwa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria kutembelea Mradi huo ambao utatoa ahueni kwa wanafunzi wake ambao kwa asilimia kubwa wanakaa nje ya chuo.
“Mhe. Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati napenda kutoa shukrani kwa niaba ya Mkuu wa Chuo kwa kuweza kututembelea, hii ni fursa ya pekee kwetu, vilevile napenda kumshukuru Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kuendeleza Mradi huu ambao ulikwama kwa kipindi kirefu kutokana na kukosa fedha za maendeleo za kuwezesha kukamilika kwa mradi huu,” alisema Bw. Chuwa.
Alibainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo wa Bweni kutawezesha kupunguza idadi wanafunzi takribani 320 kati ya wanafunzi takribani 600 ambao wanaishi nje ya chuo kwa maana ya uraiani.
Katika siku ya pili ya ziara hiyo, Kamati hiyo imetembelea pia Mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Same, Moshi-Kilimanjaro ambao pia wameridhika nao. Vilevile wanatarajia kukagua Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga na Ukarabati wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi-Kilimanjaro na kuhitimisha ziara kwa kukagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni