Mahakama ya Tanzania imeamua kuunga mkono uamuzi ya Wakazi wa Tarafa ya Usangi wilayani Mwanga ambao wameanzisha Harambee inayojulikana kama Msalagambo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo katika eneo lao.
Hatua hiyo imefikiwa leo tarehe 17 Machi, 2022 wilayani Mwanga na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Abdallah Mwaipaya kutoa taarifa kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, walipokuwa katika ziara ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, akibainisha kuwa Wakazi wa Usangi wanataka kujenga Mahakama kwa nguvu zao.
Alisema kufuatia moyo waliouonyesha wakazi hao wa kutaka kutumia nguvu zao kujenga Mahakama ya Mwanzo katika eneo lao, Mahakama imemtuma Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo na watalaamu wake kuangalia eneo lililopangwa kujengwa Mahakama hiyo kwa ajili ya kutoa ushauri wa Kitaalamu ikiwemo kutoa ramani maalum kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.
Prof. Gabriel aliongeza kuwa mbali na utoaji wa ushauri wa Kitaalamu, Mahakama itasaidia kumalizia boma ambalo wakazi wa Taarafa hiyo watakuwa wamejenga ikiwa ni pamoja na kuezeka jengo.
“Kwakweli suala la Wakazi wa Usangi kuamua kujenga Mahakama limenifurahisha sana na ninahaidi kuwa Mahakama itaendelea kuunga mkono wakazi wa maeneo mbalimbali ambayo wataanzisha miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama kwa kutumia nguvu zao ili kuhakikisha huduma za utoaji haki zinasogea karibu na makazi yao,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Mwaipaya aliongeza wakazi wa Tarafa ya Usangi wameamua kutumia Harambee ijulikanayo kama Msalagambo kujenga Mahakama ya Mwanzo.
Alisema lengo lao ni kutaka wanapata huduma ya upatikanaji wa haki katika maeneo ya karibu badala ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mwanga, kufuatia moyo waliouonyesha ameuomba uongozi wa Mahakama kuwapa ramani ili wananchi hao waanze kujenga kulingana na vigezo vinavyotakiwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mwanga Anania Thadayo alisema wakazi wake wanataka amani na ndio maana wako tayari kujitolea kujenga majengo ya Mahakama kwa kutumia nguvu zao ili wawe na eneo la kutafutia haki zao kwa misingi ya kisheria.
Wakati huo huo Mtendaji Mkuu wa Mahakama alisema wanatarajia
kujenga Mahakama 10 katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambayo yapo mbali na hayafikiki
kirahisi.
Alisema sanjari na hilo watajenga nyumba za kuishi, watachimba kisima na kuweka umeme wa jua katika nyumba hizo ili kuwa na mazingira rafiki kwa watumishi watakaopelekwa kutoa huduma kwa wananchi.
Aliongeza kwa kwa Tarafa ambazo mazingira yake ya kijiografia ni makubwa watapata fursa ya kuwa na Mahakama za mwanzo mbili ili kuwapunguzia aza wananchi wanaoishi mbali kupata huduma kwa karibu.
Lengo la Mahakama ni kuhakikisha kuwa kusiwepo eneo hapa nchini ambalo wananchi watakosa huduma ya kupata haki kwa sababu ya mazingira kuwa mbali na kutokufikika kirahisi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Emmanuel Mwakasaka (katikati) akizungumza wakati wa kikao kati ya Viongozi wa Mahakama na Kamati hiyo walipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Mwanga unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu. Kulia ni Naibu Waziri ya Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda na kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Abdallah Mwaipaya.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga Anania Thadayo (aliyesimama) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni