· Yashauri Taasisi za Umma kuiga mfano wa Mahakama
Na Tiganya Vincent, Mahakama-Arusha
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeipongeza Mahakama ya Tanzania katika ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki ambavyo vimesogeza huduma mbalimbali karibu na wananchi huku akizishauri Taasisi Taasisi za Umma kuiga ujenzi huo ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi ndani ya jengo moja.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 18 Machi, 2022 Mjini Arusha na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa ziara yao ya kutembelea na kukagua Mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jijini humo.
Mhe. Khadija Shabani (Keisha) mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo amesema kuwa hatua iliyochukuliwa na Mahakama ya ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita (6) katika Mikoa minne (4) hapa nchini imewasaidia wananchi kuokoa fedha na muda wanapofuatilia mashauri yao kwa kupata huduma za ngazi mbalimbali katika eneo moja.
Mhe. Khadija alizishauri Taasisi za umma ikiwemo Serikali za Mitaa zinatakiwa kuweka utaratibu wa kuwa na Jengo katika sehemu moja ili kuwasaidia wananchi kutotumia fedha nyingi wanapofuatilia huduma za kijamii kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kujipatia maendeleo.
“Huu mfumo wa kuhakikisha mwananchi anapata huduma katika eneo moja upo hata katika Nchi zilizoendelea kama vile China…ni vema Taasisi nyingine nazo ziige Mahakama ya Tanzania wakati wanapojenga majengo yao ili kuwarahisishia wananchi kutumia muda mrefu kufuatilia huduma badala yake watumie katika shughuli za kujiingizia kipato” amesisitiza.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Vituo Jumuishi vimekuwa msaada kwa wananchi kupata huduma ya haki katika eneo moja kuanzia ngazi ya chini hadi juu.
Amesema mwanachi kwa kutumia Vituo Jumuishi anaweza kufungua shauri katika Mahakama ya Mwanzo katika eneo hilo na asiporidhika hana haja ya kusafiri mbali anakata Rufaa katika Jengo hilohilo katika Mahakama inayofuata.
Prof. Ole Gabriel amesema hadi hivi sasa Mahakama ya Tanzania imejenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki 6 katika Mkoa wa Arusha, Mwanza, Morogoro, Dodoma na Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni).
Amesema lengo la Mahakama ni kujenga vituo vingine 12 ili kila Kanda hapa nchini iwe na Kituo hicho na kuwawekea mazingira rafiki wananchi kutafuta haki kwa gharama nafuu na muda mfupi.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Suma Ikenda Fyandomo ameipongeza Mahakama kwa kujenga majengo ambayo yameweka maeneo maalumu kwa ajili ya wanawake wanaonyenyesha ili kulinda utu wao.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria walipotembelea jengo la IJC Arusha kwa ajili ya kulikagua.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Emmanuel Mwakasaka akizungumza jambo.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Emmanuel Mwakasaka, wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna, wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda, wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Kazungu Khatibu.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni