Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma amewataka Mawakili wa
Serikali na wale wa Kujitegemea kuwa na hofu ya Mungu na kuzingatia maadili
wanapotekeleza wajibu wao kuwezesha wananchi kupata haki zao kwa wakati.
Mhe. Matuma alitoa wito
huo hivi karibuni kwenye kikao kazi kilichowaleta pamoja wadau wa Mahakama kutoka
katika Kanda hiyo, wakiwemo Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea.
Kikao hicho kilichofanyika katika jengo la Mahakama Kuu Shinyanga.
Aidha, Jaji Mfawidhi
huyo aliwataka Mawakili wote kuzingatia Sheria na kuheshimu viapo vyao ili wasiwe
chanzo cha wananchi kutopata haki zao za msingi kwa wakati ambazo wanastahili.
“Wapo baadhi ya Mawakili
wamekuwa ni chanzo cha uvunjaji wa haki za wananchi kwa maslahi yao binafsi. Napenda
asitokee Wakili katika Kanda yetu ya Shinyanga atakayekuwa chanzo cha uvunjaji
wa maadili kwa kutomtenda haki anayostahili kupata mwananchi,” alisema Jaji Matuma.
Mhe. Matuma pia aliwasisitiza
wadau waliohudhuria kikao hicho kutoshiriki vitendo vya rushwa ambavyo kimsingi
ni chanzo kikuu cha ukosefu wa haki kwa wananchi na kuwahimiza Mawakili kuwa na
dhamira ya kweli katika kutenda haki bila kumuonea mtu yeyote.
Kadhalika, Jaji
Mfawidhi huyo aliwasisitiza Mawakili wote kutokuwa chanzo cha kuahirisha mashauri
mahakamani pasipokuwa na sababu za msingi na zenye ushawishi, huku akimtaka kila
mmoja kuhakikisha anatunza kumbukumbu za tarehe za mashauri yake.
Alisema kuwa utaratibu
huo utaepusha mgongano wa tarehe, jambo linalopelekea mashauri kuahirishwa mara
kwa mara na kuongeza mrundikano mahakamani. “Kuahirisha shauri mara kwa mara
hupelekea kuwa na mlundikano mahakamani, hali inayosababisha wananchi kuchelewa
kupata haki zao kwa wakati,” alisema.
Mhe. Matuma pia
aliwasisitiza Mawakili hao kufika mahakamani kwa muda uliopangwa wa kuanza kwa
shughuli za Mahakama ili kuwezesha kila shauli kuanza kusikilizwa kwa wakati.
Kwa upande mwingine,
Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza maafisa wanaotoa msaada wa kisheria kwa
wananchi wajulikanao kama ‘Paralegals’ kufanya kazi zao za msingi kama inavyotakiwa
na siyo vinginevyo.
Alibainisha kuwa wapo
baadhi yao wamekuwa wakifanya kazi za uwakili na kusahau majukumu yao ya msingi
ya kutoa msaada wa kisheria ambayo wameelekezwa kwa mujibu
wa sheria inayowaongoza.
Naye Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Hussein Mushi amewasisitiza wadau wote wa Mahakama kufanya kazi kwa
ushirikiano wa karibu na Mahakama ili kutimiza lengo la utoaji haki kwa wakati.
Wadau waliohudhuria
kikao kazi hicho ni kutoka Ofisi ya Wanasheria Mkuu wa Serikali, Wenyeviti wa
Mabaraza ya Ardhi, Maafisa wa Baraza la Usuluhishi, Mawakili wa Kujitegemea, Maafisa
kutoka Vituo vya Msaada wa Kisheria, Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa
Huduma kwa Jamii kutoka Kanda ya Shinyanga.
Washiriki hao walipongeza
kikao kazi hicho kwani kitaleta matokeo chanya katika kufikia lengo la Mahakama
la utoaji haki kwa wakati. Wadau hao wameomba Mahakama kuendelea kuwa na vikao
kazi hivyo kwa ajili ya kufanya tathmini ya utendaji kazi katika kufikia lengo
la utoaji haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma (katikati) akiongea na
wadau wa Mahakama wakati wa kikao kazi kilichofanyika hivi karibuni. Kushoto ni Jaji wa
Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Seif Kulita na kulia ni Mtendaji wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti.
Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Shinyanga, Mhe Seif Kulita
(katikati) akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi hicho.
Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe Hussein Mushi (aliyesimama) akifafanua
jambo wakati wa kikao kazi cha wadau wa Mahakama.
Mwendesha Mashtaka wa
TAKUKURU Shinyanga, Bw. Sengoka Mndambi akichangia hoja wakati wa kikao kazi
kilichofanyika Mahakama Kuu Shinyanga.
Sehemu ya Mawakili
wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe
Athuman Matuma (hayupo katiia picha) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika
jengo la Mahakama Kuu Shinyanga.
(Picha na Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni