· Watanzania watakiwa kukitumia kutoa maoni/malalamiko
Na Tiganya Vincent, Mahakama-Tanga
Wananchi wametakiwa kutumia Kituo cha Utoaji taarifa (call center) cha Mahakama ya Tanzania kutoa maoni na malalamiko yao pale ambapo wataona hawajaridhika na huduma waliyopatiwa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ameyasema hayo mkoani Tanga alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambayo iko katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya Mahakama.
Amesema lengo la Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuagiza uanzishwaji kwa Kituo hicho ni kuhakikisha haki inatolewa kwa uwazi na uhakika kwa muda wote na kwa watu wote hapa nchini.
Prof. Ole Gabriel ameongeza kuwa huduma hiyo inapatikana katika namba ya simu ya mkononi ya 0752 500 400 na barua pepe ya maoni@judiciary.go.tz kwa saa 24 mwaka mzima ambapo watoa huduma watawasikiliza na kuwapa majibu sahihi kulingana na maswali yao.
Ameongeza kuwa Kituo hicho ni muhimu kwa wananchi kukitumia katika kuuliza maswali na kupata majibu ambayo yatawawezesha kuondoa maswali waliyo nayo ambayo mengine yanasababishwa kwa baadhi yao kutokuwa na uelewa wa kutosha yanayosababisha kufanya uamuzi usio sahihi.
“Kuwa na miundombinu bora na watumishi ni jambo moja ni lazima tuwe na jamii iliyoelimishwa kutii sheria bila shuruti na endapo kuna jambo ambalo limetokea katika jamii na hukuridhika nalo tafadhali wasiliana na Kituo hicho badala ya kuchukua Sheria mkononi” alisisitiza Mtendaji huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni