Jumanne, 15 Machi 2022

UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA MKINGA KUKAMILIKA APRILI MWAKA HUU

Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania

Ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga ambalo litagharimu shilingi bilioni 1.1 hadi kukamilika kwake unatarajia kukamilika mwishoni mwa Mwezi wa Aprili mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa leo Mjini Tanga na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambayo iko katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya Mahakama.

Amesema kukamilika kwa Jengo hilo itakuwa faraja kwa wananchi wa Wilaya hiyo na kuuwezesha Mkoa wa Tanga kuwa na Mahakama kila Wilaya.

Prof. Gabriel aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inaoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Mahakama ya Tanzania fedha za  kuboresha miundombinu kwa ajili ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Tunamshukuru Mama yetu Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuitazama Mahakama ya Tanzania kwa jicho la pekee ambapo anaendelea kutuwezesha kutupa fedha za kujenga majengo mbalimbali ikiwemo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania mjini Dodoma ambayo itamalizika Desemba mwaka huu na itagharimu bilioni 129.7” aliongeza.

Prof. Gabriel amesema kukamilika kwa majengo hayo mjini Dodoma yatafanya Mahakama ya Tanzania kuwa na majengo mazuri na ya kisasa kwa upande wa Afrika Mashariki na kwa Nchi za SADC.

Aidha Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama ya Tanzania ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita iko katika hatua za mwisho ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji haki tisa hadi 12 katika Kanda mbalimbali hapa nchini.

Amesema mpango huo wa kujenga vituo 12 ukikamilika utafikisha 18 na kuwezesha kila Kanda kuwa na Kituo kimoja baada ya vile Sita ambavyo vimeshajengwa.

Prof. Gabriel ameongeza kuwa wanatarajia kujenga Mahakama za Mwanzo 60 kwa ajili ya kusogeza huduma hiyo katika maeneo ambayo hayajafikiwa.

Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Geofrey Pinda amesema Serikali itahakikisha ifikapo mwaka 2025 Wilaya zote ziwe na huduma ya Mahakama ya Wilaya ili kusogeza huduma za utoaji wa haki karibu na wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akitoa maelezo ya masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria waliotembelea Mahakama Kuu Kanda ya Tanga kwa ajili ya ziara ya ukaguzi wa Mradi wa Jengo la kuhifadhia kumbukumbu za Mahakama.

 

 

 

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni