Jumanne, 15 Machi 2022

KAMATI YA KATIBA NA SHERIA YAIPONGEZA MAHAKAMA

·       Yapongeza matumizi ya TEHAMA

·       Uboreshaji wa miundombinu ya majengo

Na Mary Gwera, Mahakama-Tanga

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeupongeza Mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kupiga hatua katika uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake na matumizi ya TEHAMA.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 15 Machi, 2022 katika jengo la Mahakama Kuu Tanga, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Emmanuel Mwakasaka (Mb.) amesema kwa niaba ya Kamati hiyo kuwa huduma mbalimbali za Mahakama zimeendelea kuboreshwa hali ambayo inaleta faraja kwa Serikali kuona tija ya fedha inazotoa kwa Mhimili huo.

“Napenda pia kumshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuujali hasa huu Mhimili wa Mahakama kwa kuendelea kutoa fedha katika kuwezesha kuboresha huduma za utoaji haki na haki kuonekana kutendeka kwa wananchi, na ninaomba nikiri wazi kuwa Mahakama imepiga hatua kubwa sana katika matumizi ya TEHAMA na  kwa sasa inaongoza kwa Tanzania kwa sababu inakwenda kidijitali zaidi,” alisema Mhe. Mwakasaka.

Mhe. Mwakasaka sambamba na Wabunge wenzake wa Kamati hiyo, leo wameaanza ziara ya kukagua Miradi ya Mahakama ambapo wameanza rasmi kwa kukagua Jengo jipya la kuhifadhi Kumbukumbu za Mahakama lililopo Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga.

Mhe. Mwakasaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maadili, Madaraka na Haki za Bunge alikiri wazi kuridhishwa na muonekano wa jengo hilo baada ya kulikagua na Wanakamati wenzake na kusema kuwa jengo ni zuri na litasaidia katika kuhifadhi vizuri kumbukumbu za Mahakama katika Kanda hiyo.

“Leo tumekuja kutembelea jengo hili ya kuhifadhi kumbukumbu, kwakweli jengo hili kwa kiasi kikubwa linaridhisha ukiachia mbali mambo madogo madogo ambayo Viongozi wameahidi watayafanyia kazi. Na nikiri wazi kuwa Mahakama mnaendelea vizuri,” aliongeza Mbunge huyo.

Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda ameeleza kuwa wajibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ni kupitia/kukagua Miradi iliyopo chini ya mwamvuli wa Wizara hiyo ambamo ndani yake imo pia Mahakama ya Tanzania inayotekeleza Miradi mingi.

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda, alisema hadi kufikia 2025 Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inaendelea kusogeza huduma za miundombinu ya majengo huku akieleza kuwa Wilaya zote zitakuwa na Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo kwa kila Tarafa.

“Tunao uhaba mkubwa wa majengo ya Mahakama, ukiangalia katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo, kati ya Kata karibia 3800 ni Kata 960 pekee zenye Mahakama za Mwanzo, hivyo lengo lililopo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 kila Wilaya iwe na Mahakama na kwa upande wa Mahakama za Mwanzo angalau kila makao makuu ya Tarafa kuwe na Mahakama,” alieleza Mhe. Pinda.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameishukuru Kamati hiyo kwa ushirikiano na vilevile kuishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa rasilimali fedha zinazowezesha kuendesha miradi na shughuli mbalimbali za kimahakama akiongeza kuwa Mahakama ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga na kuwezesha mkoa huo kuwa na Mahakama za Wilaya kwa wilaya zake zote.

“Kwa niaba ya Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania napenda kutoa shukrani zangu kwenu ninyi Wahe. Wabunge kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mhimili huu unaotuwezesha kusonga mbele, vilevile pokeeni shukrani hizi kutoka kwa Mhe. Jaji Mkuu ambaye anatambua ziara hii ambayo mmeianza leo na ninaomba kuwahakikishia kuwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga utakamilika mwisho mwa mwezi Aprili mwaka huu,” alisema Prof. Ole Gabriel.

Jengo hilo la kisasa la Kuhifadhi kumbukumbu za Mahakama lililokaguliwa limegharimu kiasi cha fedha za Kitanzania 139, 411,376/= na imeelezwa kuwa litasaidia kuongeza ufanisi katika kazi kwa kuokoa muda mrefu wa kutafuta majalada ambayo awali hayakuwa katika mpangilio mzuri, vilevile litasaidia kuleta uwazi na kuimarisha usalama wa kumbukumbu hizo muhimu.

Kamati hiyo inatarajia kufanya ukaguzi pia kwenye Mradi wa Ujenzi wa Bweni la Wavulana katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) -Lushoto, Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Same, Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga na Ukarabati wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi-Kilimanjaro na mwisho Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Arusha.

 

 Sehemu ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia wasilisho la Mradi wa Jengo la Kuhifadhia kumbukumbu. Wasilisho hilo limetolewa leo tarehe 15 Machi, 2022 na Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji wa Mahakama, Bw. Erasmus Uisso (hayupo katika picha) wakati Wanakamati hao walipokagua Mradi huo.

Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji wa Mahakama, Bw. Erasmus Uisso akiwasilisha mada kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria (hawapo katika picha).

 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipokuwa wakikagua Jengo la kuhifadhia Kumbukumbu za Mahakama lililopo Mahakama Kuu Tanga.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kukagua Jengo la kuhifadhia Kumbukumbu za Mahakama lililopo Mahakama Kuu Tanga. Kushoto (mwenye suti ya bluu) ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda na katikati ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Emmanuel Mwakasaka na waliopo nyuma ni sehemu ya Wajumbe wa Kamati hiyo. Kamati hiyo imeanza ziara ya kukagua Miradi mbalimbali ya Mahakama leo tarehe 15 Machi, 2022.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel akionyesha moja ya maboksi maalum yanayotumika kuhifadhia majalada mbalimbali yanayohifadhiwa katika jengo hilo.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Emmanuel Mwakasaka akizungumza jambo katika hafla hiyo.

Baadhi ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakitoa maoni mbalimbali mara baada ya kukagua Jengo la kuhifadhia Kumbukumbu za Mahakama lililopo Mahakama Kuu Tanga.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni