Jumanne, 15 Machi 2022

WANANCHI MOROGORO KUNUFAIKA NA ELIMU YA SHERIA KILA WIKI

 Na Evelina Odemba - Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe leo tarehe 15 Machi, 2022 amezindua kipindi kitakachotumika kutoa elimu ya sheria kwa wananchi wanaofika kupata huduma  katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Mkoani hapa.

Hafla ya uzinduzi wa kipindi hicho ambacho kitakuwa endelevu imehudhuliwa na Mahakimu, ambao pia ni wajumbe wa kamati ya elimu, wananchi, wadau mbalimbali pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama.

Akifafanua namna Mahakama ilivyojipanga kuhakikisha wanawafikia wananchi wengi zaidi, Mhe. Ngwembe alisema kuwa wanaamini wananchi wakipata elimu sahihi ya sheria itasaidia kupunguza na hata kuondoa kabisa mashauri mengi amabayo huchangiwa na wahusika kutokuwa na uelewa kuhusu jambo husika.

“Sisi Mahakama ya Morogoro tumejitoa muhanga tuwafundishe elimu ya sheria, tutaitoa hapa mahakamani na kupitia vyombo vya habari vilivyopo Mkoani hapa kwa muda wa mwaka mzima” alisema na kuongeza, “tumesomeshwa kwa kodi za wananchi, hivyo tutatoa elimu hii ya sheria bure kama fadhira.”

Aliongeza kuwa mbali na kutumia vyombo ya habari vilivyojitolea ili kufanikisha jambo hilo pia wametenga siku tatu kwa wiki kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi na elimu hiyo itatolewa kwenye ukumbi wa mapumziko ulipo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki.

Jaji Mfawidhi huyo amezutaja siku husika kuwa ni Jumanne, Jumatano na Alhamisi kuanzia saa 2.00 Asubuhi mpaka saa 3.00 Asubuhi ambapo wananchi watapata fulsa ya kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo mifumo ya Mahakama, ndoa, mirathi, talaka na mambo mengine.

Ikumbukwe kuwa mara baada ya uzinduzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki tarehe 6 Oktoba, 2021, Mhe. Ngwembe alikutana na wamiliki 12 wa vyombo vya Habari Mkoani Morogoro na kukubaliana kutenga muda wa kipindi ili kitumike kutoa elimu ya sheria, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na tayari vyombo hivyo vinatumika mpaka sasa kwa jambo hilo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe (aliyesimama) akitoa elimu ya sheria kwa wananchi waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki leo tarehe 15 Machi, 2022 kwa ajili ya masuala mbalimbali yanayohusu haki.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe (mwenye tai nyekundu)  akiwa amezungukwa na wananchi waliojitokeza ili kupatiwa elimu ya sheria.

Kutoka kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe.  Messe Chaba, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Mhe.  Robert Kasele na Hakimu Mahakama ya Mwanzo, Mhe.  Kisaki wakifuatilia uzinduzi wa utoaji elimu ya sheria.


Sehemu ya wananchi wakifuatilia elimu  ya sheria toka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe ( hayupo pichani). Picha ya chini inamwonyesha mwananchi mmoja akiulizwa swali.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni