Na Lydia Churi-Mahakama, Tanga
Tume ya Utumishi wa Mahakama imewaagiza
Mahakimu na watendaji wote nchini kutochelewesha mashauri mahakamani bila ya
sababu za msingi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati
akihitimisha ziara ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama mwishoni mwa wiki
mjini Tanga, Kaimu Mwenyekiti wa Tume huyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe.
Dkt. Gerald Ndika amesema Mahakama inakabiliwa na changamoto ya mashauri
kutomalizika kwa wakati mahakamani changomoto ambayo pia inasababishwa na
upelelezi wa mashauri kutokamilika kwa haraka.
“Tumewashauri wadau husika
wakatafakari vizuri ili shauri linapofikishwa mahakamani upelelezi wake uwe
umekamilika na siyo kuletwa na kuegeshwa mahakamani kusubiri upelelezi”,
alisema Jaji Ndika.
Alisema katika ziara ya wajumbe wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama baadhi ya wadau waliishauri Mahakama ya Tanzania
kuhakikisha kuwa suala la utoaji haki linapewa uzito unaostahili kwa kuwa lina
uhusiano mkubwa na usalama wa taifa
katika ngazi zote yaani wilaya, Mkoa na Taifa.
Akifafanua kuhusu ziara ya Tume hiyo
katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Tanga, Dkt. Ndika alisema mojawapo ya
mikakati ya Tume ya kufahamu hali halisi ya utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania
ni kufanya ziara katika mikoa mbalimbali ambazo zinaiwezesha kutoa elimu kwa Umma
kupitia wajumbe wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama pamoja na wadau
muhimu wa utoaji haki.
Alisema katika ziara hiyo, Tume
imefanikiwa kupata maoni, ushauri na kufikisha elimu iliyokusudiwa baada ya kukutana
na wajumbe wote wa Kamati za Maadili za mikoa ya Pwani, Morogoro na Tanga
pamoja na wilaya zake.
Kuhusu msongamano wa mahabusu
magerezani, ilionekana kuwa wakati Mahakama ikiendelea na jitihada za kujenga
majengo, upo umuhimu wa wadau wa Mahakama kuendelea kujenga Magereza ili
kupunguza msongamano.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha Kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama Mkoa wa Tanga pamoja na wilaya zake wakiwa kwenye Mkutano wa Tume uliomalizika mwishoni mwa wiki mjini Tanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni