Na Innocent Kansha - Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amewakumbusha watumishi kutumia taaluma
zao vizuri, kufanya kazi kwa Uadilifu bila upendeleo, kuongeza uwazi na
mshikamano mahala pa kazi bila kuathiri maelekezo ya viongozi ili kusaidia
kufanikisha malengo ya Mpango Mkakati wa awamu ya pili.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa awamu ya
pili 2020/2021 hadi 2024/2025 na huduma
kwa mteja kwa watumishi
wote wa divisheni hiyo leo tarehe 12 Machi 2022, katika Ukumbi
wa Mafunzo Kisutu jijini Dar es salaam, Mhe.
Maghimbi amesema, anatambua kwamba
katika safari ya uboreshaji wa huduma za Mahakama unasimamia nguzo tatu, (3) ambazo ni Utawala bora na
usimamizi wa rasilimali watu, Utoaji haki sawa na kwa wakati na Ushirikishwaji
wa wadau.
“Naelewa ilivyo ngumu kujenga jamii yenye uadilifu,
kwani misingi ya uadilifu hujengwa kuanzia kwa wazazi wetu na walezi wetu,
lakini kamwe hili haliwezi kutufanya tukaacha kukumbushana wajibu wetu kama
wadau namba moja wa utoaji haki”, alisema Jaji Mfawidhi
Jaji Maghimbi ameongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo
yatawajengea uwezo watumishi kufahamu mikakati ya Taasisi, kuwaongezea watumishi
uadilifu na pia kuwapa hamasa ya kutoaji huduma za kimahakama zinazoridhisha na hivyo
kuimarisha ushirikiano wa watumishi katika kuboresha huduma.
Aidha, Jaji Mfawidhi aliwasisitiza washiriki kuwa mada
zilizoandaliwa ni muafaka na zitasaidia kuwajengea uwezo watumishi wa kusimamia na
kutekeleza nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama ambao ndiyo jukumu la
msingi lililowekwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama
ilivyofanyiwa marekebisho mara kadhaa.
“Inanipa faraja kubwa kusema uboreshaji wa huduma unaoendelea
katika Taasisi yetu hauna budi kupongezwa na kuungwa mkono na kila mmoja wetu.
Ni dhahiri kwamba kila mmoja analo la kusimulia kwa kuangalia tulipotoka na
mahali tulipo sasa, ni wazi kwamba ilikuwa ni nadra sana kupata fursa kama hii
ya kukutana kwa wingi wetu kama ilivyo sasa na kupata mafunzo”, alisema Jaji
Maghimbi
Jaji Mfawidhi, alisema kuhusu
Taarifa ya REPOA ni tafiti inayotoa tathmini iliyofanyika kwa Mahakama kupima huduma zinazotolewa ili
kujua ni kwa kiasi gani zina kidhi viwango,
hilo litasadia kupima na
kurekebisha pale ambapo hapakwenda sawa kama
taratibu za utoaji huduma zinavyopaswa.
“Maoni yaliyotolewa juu yetu isiwe sehemu ya
kuwachukia wateja wetu bali iwe chachu ya mabadiliko, kibinadamu huwezi
kutambua unapokosea isipokuwa kupitia watu wengine”.aliongeza Jaji Maghimbi
Kwa upande wa matarajio ya mafunzo hayo Mhe. Maghimbi alisema,
ni imani kubwa baada ya mafunzo hayo watumishi watabadili mienendo yao binafsi na kushirikiana
vizuri na wadau wote, kuwa waaminifu
na wakweli katika utoji wa huduma. Kutotoa huduma kwa upendeleo na kuimarisha
ushirikiano “team work”. Kuongeza
uwajibikaji na uwazi kwa kulinda
uhuru wa Mahakama.
Jaji Maghimbi alihitimisha kwa kuwashukuru Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa mchango wake mkubwa wa kufanikisha mafunzo hayo “Nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitatoa shukrani za dhati kwa wawezeshaji wa mafunzo haya Shirika la Kazi duniani na wale wote ambao wameshiriki katika maandalizi ya mafunzo haya”,.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni