Ijumaa, 11 Machi 2022

WAZIRI SIMBACHAWENE ATETA NA JAJI MKUU MATUMIZI YA KISWAHILI MAHAKAMANI

 

Na Faustine Kapama, Mahakama

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene leo tarehe 11 Machi, 2022 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dar es Salaam na kufanya  mazungumzo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Aidha, Mhe. Simbachawene, ambaye aliongozana na Naibu Waziri, Mhe. Geofrey Pinda, Katibu Mkuu Mary Makondo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Kazungu Khatibu alipokea taarifa mbili za usikilizaji wa mashauri na utekelezaji wa uboreshaji wa Mahakama zilizowasilishwa na viongozi waandamizi wa Mhimili huo.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Simbachawene alimweleza Jaji Mkuu kuwa Wizara yake imeshaanza kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili sheria 250 kati ya 460 zilizopo na mchakato kama huo unaendelea katika sheria zingine, lengo likiwa kuongeza uelewa wa wananchi katika sheria na uendeshaji wa mashauri.

“Tunataka kuwe na matumizi ya Kiswahili yanayoonekana, wananchi wanalisubiri hili kwa hamu sana. Matarajio ni makubwa na baada ya muda, Bunge la kuanzia mwakani kutakuwa na maswali mengi. Kwa upande wetu tumezishirikisha taasisi ambazo zinasimamia sheria na wamejitahidi kwa kiasi kikubwa. Takribani sheria 250 kati ya 460 zimefikia hatua ya juu katika kutafsiri,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu alimweleza Mhe. Simbachawene kuwa Mahakama imepiga hatua kubwa katika suala hilo ambapo Kamati ya Kanuni imefanya tafsiri ya karibia sheria zote ambazo hutumika mahakamani, hasa zile ambazo zipo chini ya mamlaka ya Jaji Mkuu, ambapo Majaji na Mahakimu walishiriki kikamilifu.

“Mahakama imeshakubali kuwepo kwa suala hilo kwa kuangalia historia ya matumizi ya lugha, Mahakama za Mwanzo, ambazo hutumiwa na Watanzania kwa asilimia70 hutumia Kiswahili bila tatizo lolote. Changamoto imekuwa katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ambazo ni Mahakama za kumbukumbu,” alisema.

Kuhusu lugha ya Kiingereza, Jaji Mkuu alimweleza Waziri kuwa Mahakama ipo katika Jumuiya ya Madola ambapo uamuzi unaotolewa hutumika kwa kiasi kikubwa kwenye nchi katika jumuiya hiyo na hazina kubwa ya elimu ya sheria ipo kwenye kumbukumbu ambazo zipo kwenye lugha hiyo.

“Kwa hiyo, sisi tunatafuta teknolojia itakayomwezesha mwananchi kuchagua lugha anayoitaka (kama ilivyo India). Mahakama inaweza kuandika hukumu yake kwa Kiingereza lakini ile teknolojia inamwezesha mwananchi kupata kwenye lugha anayotaka. Tumewasiliana na India na tumegundua teknolojia yao wanayoitumia waliipata Italia. Tumeunda timu ya wataalamu, walienda Italia kujifunza. Kwa sasa timu hiyo inaendelea kutayarisha hiyo teknolojia,” alisema.

Baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Simbachawene alipata wasaa wa kuongea na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikia katika suala hilo la kutafsiri sheria kwa lugha mbalimbali. Alisema Serikali itahakikisha wanakamilisha mchakato huo ili kuwasaidia wananchi kuelewa sheria zilizopo kwa lugha rahisi.

“Serikali imeendelea kutafsiri sheria mbalimbali kati ya sheria 460,  sheria 250  zimefikia hatua ya juu katika kutafsiri. Tunaipongeza mahakama kwa kwenda mbali zaidi kwa kuweka mfumo wa kutafsiri sheria kwa lugha tofautitofauti,’’ Waziri huyo alisema.

Aidha, Mhe. Simbachawene alibainisha kuwa Mahakama ni Mhimili ambao unapaswa kujitegemea katika utoaji haki, hivyo haupaswi kuingiliwa na chombo chochote.

‘’Tuna Mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama hivyo katika utendaji kazi wa kila mamlaka au mhimili unapaswa kufanya kazi kila mmoja bila kuingiliana. Nimepata fursa nzuri ya kuzungumza na Jaji Mkuu kuhusu mambo yanayofanywa na Mahakama,’’ alisisitiza.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha alisema  mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kutoa urahisi na uelewa kwa wananchi kuhusu sheria za nchi ambazo kwa miaka mingi zilizokuwa zinatumika ni za lugha ya Kiingeleza.

Alisema lengo la kutafasiri sheria nyingi ni kutoa uelewa wa kutosha kwa wananchi ambapo Mahakama imetafuta teknolojia itakayosaidia kuhamisha sheria hizo kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili ili wananchi  waelewe uamuzi wa Mahakama kwa lugha rahisi.

“Changamoto tunazokutana nazo ni kupata misamiati sahihi ya Kiswahili kwa sababu ya uwepo wa vurugu kubwa ya maneno mengi yasiyorasmi, jamii ielimishwe kujitahidi kutumia lugha fasaha ili mifumo tunayotafuta ya kusaidia kutoa lugha, iweze kutoa lugha sahihi,’’ alifafanua Bw. Magacha.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene na viongozi alioongozana nao kutembelea Makao Makuu ya Mahakama jijini Dar es Salaam leo tarehe 11 Machi, 2022.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene akisaini kwenye kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye ofisi ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma.
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi akizungumza wakati wa kikao kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene kilichofanyika ofisini kwa Jaji Mkuu jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji wa Huduma za Mahakama, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akitoa mada ya uboreshaji wa huduma za Mahakama mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene (hayupo katika picha).

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pindi Waziri huyo alipomtembelea Jaji Mkuu leo tarehe 11 Machi, 2022 ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene (kushoto). Kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina. Waliosimama nyuma ni baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mkuu wa Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. George Simbachawene (kushoto), kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina. Waliosimama (wa pili kushoto) ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda, wa pili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Mary Makondo, wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Kazungu Khatibu na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Solanus Nyimbi.

(Picha na Mary Gwera-Mahakama)


Maoni 1 :

  1. In fact, I commend the legal sector in Tanzania, as it is making daily progress in improving the judiciary. ranging from buildings, court officials and even applicable laws. for example such a transition to the mother tongue (Kiswahili). In fact, this is a very important and important issue, whereas from this change of language in court will increase the public's confidence in the defense or prosecution of the courts.
    so let me take this opportunity to congratulate the Chief Justice of Tanzania Hon. prof. Ibrahim Hamis Juma also I commend the ministry of constitution and law for the good work they are doing

    JibuFuta