Na Lydia Churi- Mahakama, Morogoro
Kaimu
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika amesema utoaji haki kwa wakati ni muhimu katika kujenga
uchumi imara na shindani utakaowezesha Tanzania kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo
ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza
kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wajumbe wa Kamati za Maadili
ya Maafisa wa Mahakama za Mkoa na Wilaya jana mjini Morogoro, Jaji Ndika
alisema kuwa eneo la utoaji haki lina umuhimu mkubwa katika kujenga uchumi
imara hivyo ni jukumu la Tume ya Utumishi wa Mahakama kujenga ufanisi wa
shughuli za utoaji haki.
Kaimu
Mwenyekiti huyo alisema huduma ya msingi ya utoaji haki inayotolewa na Mahakama
ya Tanzania ni ya ustawi wa wananchi kwa lengo la kujenga utawala bora.
Alisema
katika kujenga utawala bora, Mahakama ina wajibu wa kutatua migogoro inayotokea
katika jamii. Akitolea mfano wa migogoro ya ardhi, Jaji Ndika alisema kama
itakuwa mingi na isipotatuliwa inaweza kusababisha Mkoa kutotawalika kwa urahisi,
hivyo huduma zinazotolewa na Mahakama zinalenga katika kujenga utawala bora.
“Ili
kujenga utawala bora, kazi mojawapo ya Mahakama ni kuhakikisha haki inatolewa
kwa wakati”, alisisitiza Jaji Ndika ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama.
Wakati
huo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Temeke, Mhe. Ilvin
Mugeta, ambaye amealikwa na Tume kutoa elimu amesema Watumishi wa Mahakama ya
Tanzania wanao wajibu wa kufahamu haki na wajibu wao ili waweze kutambua
matendo ambayo ni kinyume na maadili ya utendaji.
Alisema
kwa kutambua matendo hayo, Watumishi hao watasaidia kuongeza tija katika kazi
zao za kila siku, kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama na kuongeza imani ya
wananchi kwa Mhimili huo.
Jaji
Mugeta alisema Watumishi wa Mahakama wana jukumu la kufahamu haki na wajibu wao
kwa kuwa kuna changamoto kwa Watumishi hao ya kutofahamu ipasavyo haki na
wajibu wao kwa taasisi.
Alisema
wapo Watumishi ambao hawafahamu taarifa muhimu na sahihi zinazohusu kazi zao. “Changamoto
hizi huweza kutatuliwa kwa kuwafahamisha na kuwashauri kusoma nyaraka
mbalimbali ili kufahamu sheria za utumishi na masuala mbalimbali yanayohusu
Mahakama,” alisema.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama inaendelea na ziara yake katika mkoa Tanga baada ya
kukamilisha kwenye mikoa ya Pwani na Morogoro. Lengo la ziara ni kuitangaza
Tume hiyo, kutoa elimu na kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa
wa Mahakama za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa Mahakama ili kuboresha huduma
zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Temeke Mhe. Ilvin Mugeta akielezea Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama waliokutana na wajumbe wa Tume hiyo jana Machi 9, 2022 mkoani Morogoro.
Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika akizungumza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni