Alhamisi, 10 Machi 2022

TAWJA KIGOMA YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUTOA ELIMU

 

Na Festo Sanga-Kigoma, Mahakama

Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Kanda ya Kigoma kimeadhimisha siku ya wanawake nchini tarehe 8 Machi, 2022 kwa kutoa elimu kwa umma katika masuala mbalimbali ya kisheria.

Maadhimisho hayo yalifanyika kimkoa katika Wilaya ya Uvinza, Kata ya Kazuramimba ambapo mgeni raismi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Ester Alexander Mahawe aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa.

Katika maadhimisho hayo, chama hicho kwa kushirikiana na watumishi wanawake wa kada mbalimbali kilijikita zaidi katika utoaji wa elimu kwa umma kwa njia za Radio na Mabanda ya maonesho.

Akitembelea banda la maonesho la Mahakama, mgeni rasmi alikiomba Chama cha Majaji na Mahakimu kuwasaidia wanawake wa Mkoa wa Kigoma kufuatia malalamiko mengi ya wawanake katika eneo la mirathi.

“Kama Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, napokea kesi nyingi za wanawake katika eneo hili la mirathi, hivyo naomba chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake muone namna ya kutusaidia,” alisema Mhe. Mahawe.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa alisema kuwa chama kitaendelea kutoa wa elimu kwa njia ya vipindi vya radio kila Jumatano katika kila ngazi ya Mahakama, kuwaelimisha wanawake kuhusu haki zao, hususani maeneo ya mirathi, ndoa na talaka, hivyo aliwataka wanawake wote kuhudhuria vipindi hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ester Mahawe (katikakt) akipokea ufafanuzi  kutoka kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji- Kigoma, Mhe. Vestina Nombo wa huduma wanazotoa chama cha Majaji na Mahakimu Kigoma(TAWJA)  katika banda la maonesho la Mahakama lililokuwa katika eneo la maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Uvinza, Kata ya Kazuramimba. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma Mhe. Rose Kangwa

Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Kigoma wakitoa Elimu kwa njia ya radio kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma katika kituo cha Radio Joy FM.

Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Bi Veronika Paul akigawa wa vipeperushi vyenye ujumbe mbalimbali kwa akina mama waliohudhuria maadhimisho hayo.

Watumishi wa Mahakama wakiwa wamebeba bango lenye kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake nchini wakijiandaa na maandamano.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma Mhe. Rose Kangwa(wa kwanza kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wanawake wa Mahakama Mkoa wa Kigoma.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni