Na Lydia Churi- Mahakama, Morogoro
Tume
ya Utumishi wa Mahakama imetoa wito kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutekeleza
majukumu yake kwa kuongozwa na dhamira tatu ambazo ni kutenda haki, kutotumia
madaraka vibaya na kuzingatia maslahi ya Umma.
Akizungumza
katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau uliofanyika jana mjini
Morogoro, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani
amesema endapo ofisi hiyo itafanya kazi kwa kuzingatia misingi aliyoitaja,
hakutakuwa na mlundikano wa mahabusu magerezani na upelelezi utakamilika kwa
haraka kwa kuwa Waendesha mashtaka ndiyo wenye jukumu la kusimamia upelelezi wa
makosa ya jinai nchini.
Jaji
Kiongozi ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama amesema kuwa
kukamilika kwa upelelezi wa makosa ya jinai kwa muda mfupi kutaiwezesha
Mahakama kusikiliza mashauri kwa haraka zaidi na hivyo wananchi kupata haki kwa
wakati.
“Mahakama
inatarajia kuwa Waendesha Mashtaka watakapofanya kazi yao kwa weledi na kwa
kuzingatia Sheria, taratibu na miongozo iliyopo, wataisaidi Mahakama kutenda
haki”, alisema.
Alisema
Waendesha Mashtaka wanatakiwa kuwa na ujuzi wa kutosha wa Sheria na kuwa na uwezo wa kuamua juu ya hatua ya
mashauri wanayoyaendesha ikiwa kuna sababu ya kuendelea nayo au kuyaondoka
mahakamani na hivyo kusaidia haki kupatikana kwa wakati.
Jaji
Kiongozi alisema Mahakama inatarajia kuona Waendesha Mashtaka wakichukua hatua
thabiti kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao na hivyo kutokukwamisha kasi ya
usikilizwaji wa mashauri ya jinai mahakamani.
Aliwataka
kufanya uamuzi kabla ya kufikisha shauri mahakamani badala ya kulifikisha
likiwa na mapungufu mengi ya kisheria na kiushahidi. Alifafanua kuwa uamuzi wa
kulifikisha shauri mahakamani uzingatie uwepo wa ushahidi wa kutosha.
Kuhusu
Maafisa Ustawi wa Jamii ambao pia ni wadau muhimu katika usikilizwaji wa
mashauri, Jaji Siyani Mahakama inatarajia kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii watakuwa
chachu ya kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa haki na si kikwazo
Alisema
Maafisa hao hawana budi kuwepo mahakamani kwa kuwa wanayo nafasi kubwa katika
kuharakisha usilikilizwaji wa mashauri yanayowahusu watoto. Aliongeza kuwa Maafisa
hawa wasipokuwepo mahakamani hukwamisha shughuli za usikilizwaji wa mashauri ya
watoto.
Kwa
upande wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS), Mhe. Siyani alisema wanalo
jukumu la kuisaidia Mahakama kutenda haki kwa kuwa uwepo wao mahakamani
unausaidia Umma kufikia huduma za Mahakama na hivyo haki kupatikana kwa wakati.
Aidha,
ametoa rai kwa Mawakili kuwashauri wateja wao kutumia usuluhishi kama njia ya
kutatua migogoro yao kwa lengo la kupunguza gharama na kujenga jamii yenye
mshikamano, undugu na kudumisha Amani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe.
Martine Shigela ameahidi kuendeleza kushirikiano uliopo
kati ya Mhimili wa Mahakama na Serikali mkoani Morogoro ili kuwezesha wananchi
kupata haki kwa wakati.
Mkuu
huyo wa Mkoa ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuandaa Mikutano na
wadau wa Mahakama pamoja na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama
za wilaya na Mkoa kwa lengo la kutoa elimu na kubadilishana uzoefu ili
kuboresha mazingira ya utoaji haki nchini.
Wajumbe
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara katika mikoa ya Morogoro
na Tanga baada ya kumaliza ziara katika mkoa wa Pwani. Ziara hiyo ya Tume ina
madhumuni ya kuitangaza Tume hiyo, kutoa elimu na kukutana na wajumbe wa Kamati
za Maadili za mikoa na wilaya pamoja na wadau wa Mahakama ili kuboresha huduma
zinazotolewa na Mahakama.
Sehemu ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania wakiwa katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mkoani Morogoro. Kulia ni Naibu Katibu wa Tume hiyo Bibi Enziel Mtei akifuatiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Tume Bw. RickNeville Mwanri. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania Bibi. Beatrice Patrick na kushoto ni Mkurugenzi wa Ukaguzi na Maadili wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Anna Magutu.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama waliohudhuria Mkutano wa Tume na Wadau. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania Bw. Stephen Magoha.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Tume na Wadau wa Mahakama jana mkoani Morogoro.
Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili wa Kujitegemea Mhe. Genoveva Kato akizungumza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro Mhe. Paul Ngwembe akisoma Taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Mahakama kanda ya Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela akizungumza kwenye Mkutano wa Tume na Wadau wa Mahakama jana mkoani Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni