Na Francisca Swai, Mahakama-Musoma
Watumishi wanawake kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma jana tarehe 8 Machi, 2022 wameungana na wanawake wote ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea vituo vyenye watoto wenye mahitaji maalumu.
Wakiwa katika vituo hivyo, watumishi hao wametoa vitabu vinavyohusu haki za wanawake na watoto (Women Access to Justice) kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwisenge yenye watoto wenye ulemevu wa kuona na ngozi (Albino), Shule ya Msingi Mwembeni yenye watoto wenye ulemavu wa kusikia na Kituo cha kulelea watoto cha Jipe Moyo kilichoko Musoma Mjini.
Mbali na kutembelea vituo hivyo, watumishi hao wanawake wakiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Eugenia Rujwahuka pia waligawa vitabu hivyo kwa watumishi wengine wa Mahakama katika Kanda hiyo.
Aidha, watumishi hao baada
ya kutembelea vituo hivyo walishiriki katika maadhimisho ya siku ya wanawake
duniani yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Butiama, hivyo kuungana na
wanawake wengine waliohudhuria katika sherehe hizo kutoka taasisi mbalimbali
ndani ya Mkoa wa Mara.
Mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo alikuwa Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mara, Bi. Happiness Mtutwa.
Watumishi wa Mahakama Kuu musoma wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupata vitabu hivyo. Waliokaa mezani katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Frank Mahimbali na kulia ni mwakilishi wa TAWJA Kanda ya Musoma, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mhe. Prisca Mkeha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni