Na Brian Haule-Mahakama, Songea.
Aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi
amewaasa watumishi kuendeleza ushirikiano baina yao na viongozi wanapotekeleza
majukumu mbalimbali ya kimahakama ili kufikia azma ya Mahakama ya kutoa haki kwa
wananchi kwa wakati.
Kauli
kama hiyo ilitolewa na Jaji Mfawidhi mpya wa Kanda hiyo, Mhe. Yose Mlyambina
katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika jana tarehe 28 Machi, 2022 mbele ya watumishi wa Mahakama Kanda
ya Songea mara baada ya Mhe. Moshi kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala
Kuu jijini Dar es Salaam.
“Napenda
kuwajulisha imempendeza Jaji Mkuu nihamishiwe Mahakama Kuu (Masjala Kuu) Dar es
Salaam. Nawashukuru kwa ushirikiano mkubwa mlionionyesha kwa kipindi chote nilichokuwepo
hapa. Tumeishi vizuri na naomba ushirikiano mlionipa mimi mumpatie pia Mhe. Mlyambina,”
amesema Mhe. Moshi
Kwa
upande wake, Jaji Mfawidhi huyo mpya alianza kwa kumshukuru Mungu kwa kuwezesha
jambo hilo kufanyika kwani kupitia yeye imempendeza Jaji Mkuu amhamishe kutoka
Iringa hadi Songea. Amemshukuru pia Mhe. Moshi kwa ushirikiano aliomwonyesha tangu
siku ya kwanza alipofika Songea.
Alitumia
nafasi hiyo kuwaomba watumishi wote kumpa ushirikiano kwa kuzingatia yeye peke
yake hatoweza kutimiza malengo ya Mahakama yanayokusudiwa, hivyo ni muhimu
kupata mchango wa utendaji kazi kwa kila mmoja wao.
Mhe.
Mlyambina pia aliwakumbusha watumishi hao kuzingatia nidhamu katika kazi na
kuwahudumia wateja wanaofika mahakamani kutafuta haki kwa upendo. Amewasihi watumishi hao kupenda kujiendeleza, huku
akiahidi kuwaunga mkono wale watakaohitaji kufanya hivyo ili kujiongezea
maarifa katika kazi.
Kadhalika,
Mhe. Mlyambina amehimiza matumizi endelevu ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliaon (TEHAMA) katika shughuli zote za kimahakama, akiamini Songea
itaongoza kwa Mahakama Mtandao, kama ilivyokuwa Tanga kipindi fulani alipokuwa
akihudumu katika Mahakama hiyo. “Naomba Afisa Tehama uwafundishe watu wetu kama
hawana mafunzo ya Mahakama Mtandao. Tutaandaa utaratibu wa kuwafundisha hata wadau
na wateja wetu ili wote twende pamoja, hatutaki mtu abaki nyuma,” alisisitiza.
Akiongea
kwa niaba ya watumishi, Hakimu Mkazi, Mhe. Asifiwe Jembe amemshukuru Mhe. Moshi
kwa malezi yake kama kiongozi na kumkaribisha Mhe. Mlyambina kama kiongozi mpya katika Kanda hiyo.
Kwa
upande wao, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe. Sylvester Ngh’umbu
na Mtendaji wa Mahakama katika Kanda hiyo, Bw. Geofrey Mashafi waliwaasa
watumishi wa Mahakama kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na Jaji Mfawidhi mpya.
Aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi (katikati)
akiongea na watumishi katika hafla ya makabidhiano ya ofisi jana tarehe 29
Machi, 2022. Kushoto Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Yose Mlyambina na kulia ni Jaji
wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Upendo Madeha.
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina (aliyesimama) akiongea na watumishi katika hafla hiyo. Katikati ni aliyekuwa Jaji Mfawidhi katika Kanda hiyo, Mhe. Sekela Moshi akifuatiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Upendo Madeha.
Baadhi
ya Watumishi wa Mahakama wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni