Jumanne, 29 Machi 2022

WADAU HAKI JINAI KATAVI KUSHIRIKIANA KUMALIZA MLUNDIKANO WA MASHAURI

 Na James Kapele – Mahakama, Katavi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru ametoa rai kwa wadau wote wa haki jinai Mkoa wa Katavi kushirikiana ili kumaliza mlundikano wa mashauri yaliyopo mahakamani.

Akizungumza katika kikao cha kusukuma mashauri kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Ndunguru aliwaaasa wadau wote kutimiza wajibu wao ili kutokwamisha mnyororo wa upatikanaji haki pindi mashauri yanapokuwa yamewasilishwa mahakamani.

“Ninyi nyote mliopo hapa hakikisheni mnashirikiana ili kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wakati kwa wananchi. Hakimu peke yake hawezi kufanya kazi bila kushirikiana na wadau wengine. Mmoja wenu atasababisha wengine kukwama kama atashindwa kutimiza wajibu wake,” alisema.

Aliwaambia wadau hao kuwa ni aibu kuona mashauri yamekwama kusikilizwa kwa sababu mmoja ameshindwa kutimiza wajibu wake, hivyo ni muhimu kushirikiana kwa pamoja ili mashauri hayo yamalizike kwa haraka.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe Gway Sumaye amewasihi wadau wa haki jinai waliohudhuria kikao hicho kutokujiona fahari na kupelekea watuhumiwa kukaa mahabusu kwa muda mrefu kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wao.

“Sisi tunalala usingizi majumbani kwetu lakini wapo wenzetu mahabusu hawapati usingizi kwa sababu sisi tumeshindwa kutimiza wajibu wetu, mimi sitokubaliana na hili kabisa. Lazima tufanye kazi kwa maslahi mapana ya utoaji haki kwa wadau wetu ili kulinda taswira na heshima ya Mahakama” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Katavi, Bw, Mkwasi Rashid aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa kama mamlaka ya kiuchunguzi watahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha upelelezi wa mashauri kwa wakati.

Naye Mkuu wa Waendesha Mashtaka katika Mkoa huo, Bw, Abel Mwandalama amewahakikishia wadau wa haki jinai kuwa maazimio yote waliyofikiwa na Kikao hicho yanayohusu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yatatekelezwa kikamilifu.

Jumla ya mashauri 39 yaliyosajiliwa katika Wilaya za Mpanda, Mlelena Tanganyika pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi yalijadiliwa katika kikao hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga,  Mhe. Dunstan Ndunguru (aliyesimama) akifungua kikako cha wadau wa haki jinai kujadili namna ya kusukuma mashauri Katavi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe Gway Sumaye (kulia)ambaye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kikao hicho akisisitiza jambo.


Sehemu ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni