Jumanne, 29 Machi 2022

WANANCHI SHINYANGA WAIMWAGIA SIFA MAHAKAMA KWA HUDUMA BORA

 Na.Emmanuel Oguda, Shinyanga

Mahakama ya Tanzania imepongezwa kwa huduma bora inazotoa kwa wananchi katika Wilaya ya Shinyanga Mkoa wa Shinyanga.

Pongezi hizo zimetolewa jana tarehe 28 Machi, 2022 na baadhi ya wananchi mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma alipotembelea Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga na kuongea na wananchi waliokuwa wakisubiri kupata huduma za kimahakama.

“Huduma za Mahakama kwa sasa zimeboreshwa na kwa kweli ni za kuridhisha sana na matokeo yanaonekana, tunahudumiwa na kuridhika kabisa’’ mkazi mmoja wa Shinyanga alimweleza Jaji Matuma ambaye yupo katika ziara kukagua Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya katika Kanda ya Shinyanga.

Awali, Mhe. Matuma aliwasihi wananchi kutokuwa na woga wakati wanapoona huduma hazitolewi na Mahakama katika ngazi yoyoye kwa kiwango cha kuridhisha. “Tumejipanga kwa ngazi zote kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wananchi kwa kiwango cha kuridhisha,’’ alisema.

Jaji Mfawidhi huyo amewaomba wananchi wasikae kimya wanapokuwa na malalamiko ya aina yoyote, bali wafike mahakamani, ikiwezekana hata Mahakama Kuu ambapo changamoto zao zitatatuliwa kwa haraka zaidi.

Mhe. Matuma pia alitoa rai kwa watumishi wote wa Mahakama kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, amewataka Mahakimu kuhakikisha wanasikiliza mashauri kwa haraka zaidi ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati kwa wananchi wa Shinyanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma (kushoto) akizungumza na wananchi (hawapo katika picha) alipotembelea Mahakama ya Wilaya Shinyanga jana tarehe 28 Machi, 2022.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mhe. Mary Mrio (katikati) akichukua baadhi ya maagizo muhimu yaliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma wakati akiongea na wananchi.

Mmoja wa wakazi wa Shinyanga akitoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga.

Sehemu ya wananchi waliofika kupata huduma katika Mahakama ya Wilaya Shinyanga (picha ya juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma (hayupo katika picha).



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni