Na Angel Meela-Mahakama, Arusha
Aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna amewakumbusha
watumishi wa Mahakama kuendelea kuchapa kazi na kuhakikisha wananchi wanapata
haki zao kwa wakati.
Mhe.
Mzuna ametoa rai hiyo leo tarehe 28 Machi, 2022 katika hafla fupi ya kuwaaga
watumishi wanaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha mara baada
ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, Masijala Kuu jijini Dar es Salaam.
“Wananchi
ndio waajiri wetu namba moja, mwananchi ndiye anaetulipa mshahara. Mnyonge
ataonewa kama viongozi hawatasimamia haki, hivyo nawaomba mtangulize maslahi ya
wananchi kwanza mnapotekeleza majukukumu yenu,” amewaambia watumishi hao.
Mhe.
Mzuna amemkaribisha Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama, katika Kanda hiyo, Mhe. Joachim
Tiganga ambaye awali alikua Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza.
Amewasihi
watumishi wote kumpa Mhe. Tiganga ushirikiano mara kumi au hata mara sabini
zaidi ya waliompa yeye ili kuendelea kuing’arisha Kanda hiyo katika mambo
mbalimbali ya kimahakama. Mhe. Mzuna amemhakikishia Jaji Mfawidhi huyo mpya kuwa
timu nzima iliyopo katika Kituo Jumuishi Arusha inafanya kazi vizuri na kwa ushirikiano wa hali ya juu.
Jaji
Mzuna aliitumia nafasi hiyo kumpongeza Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo,
Mhe. Mohamed Gwae, kwa namna ya pekee kwa kumaliza mashauri mengi kuliko majaji
wengine kwa mwaka 2021. Mhe. Gwae alimaliza mashauri zaidi ya mia tatu katika
kipindi hicho, hatua iliyomfanya Jaji Mzuna kumpatia cheti cha pongezi.
Naye Jaji
Tiganga amemshukuru Mhe. Mzuna kwa kazi nzuri iliyotukuka aliyoifanya wakati
anaitumikia Mahakama ya Tanzania kama Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Arusha.
“Historia
yangu haiwezi kukamilika bila yeye (Jaji Mzuna) kutajwa kwa sababu wakati nateuliwa
kuwa Naibu Msajili, Mhe. Mzuna ndiye alikuwa Jaji Mfawidhi wangu,” alisema.
Mhe. Tiganga aliwaomba watumishi wote ushirikiano katika kazi na mambo
mbalimbali ya kijamii kwa vile yeye ni mgeni Arusha.
Amewapongeza
Majaji kwa kazi kubwa waliyofanya, ikiwemo kupunguza mlundikano katika Kanda ya
Arusha na kuomba waendelee kumpa ushirikiano huo na zaidi. Baada ya mazungumzo hayo,
Mhe Mzuna alikata keki ya kuagwa na Jaji Tiganga akakata keki ya kukaribishwa
kama ishara ya upendo.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akifuatilia jambo katika hafla ya kumuaga iliyofanyika leo tarehe 28 Machi, 2022.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akimkabidhi cheti Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda hiyo, Mhe. Mohamed Gwae.
Hongereni Sana Wahe. Majaji.
JibuFuta