Jumatatu, 28 Machi 2022

MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA ARDHI KUPAMBANA NA MLUNDIKANO

 Na Faustine Kapama, Mahakama

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi hivi karibuni ilifanya Kikao Maalum na wadau mbalimbali kujadili na kupanga mikakati itakayosaidia kuondoa mashauri ya mlundikano na kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Taarifa iliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Agnes Mgeyekwa inaonyesha makubaliano 22 yaliyofikiwa na Kikao hicho baada ya majadiliano ya kina, ikiwemo Majaji, Naibu Wasajili na Wenyeviti wa Mabaraza kuchukua hatua ili kudhibiti maahirisho ya mashauri yasiyokuwa ya lazima.

“Waheshimiwa Majaji, Naibu Wasajili na Wenyeviti wa Mabaraza wazingatie matumizi sahihi ya uhuru wa Mahakama na kutoa maamuzi kwa mujibu wa sheria. Hati za wito au barua za kuwaita mashahidi ambao ni watumishi wa umma zitolewe kwa wakati,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kikao hicho pia kimeazimia Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kuandika mienendo ya mashauri kwa kuzingatia sheria ili kuepusha amri za Mahakama kurudisha mashauri kusikilizwa upya na wahimizwe kuchapa mienendo hiyo na uamuzi na kuhakiki kabla ya kuwasilishwa Mahakama Kuu.

“Amri ya kuita majalada ya mashauri kutoka kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ziwafikie Wenyeviti wa Mabaraza kwa wakati ili wawasilishe majalada kwa wakati,” taarifa hiyo inaeleza moja ya maazimio yaliyofikiwa na kikao hicho.

Aidha, Kikao hicho kimeazimia Mawakili wa Serikaii na Mawakili wa Kujitegemea wakumbushwe kuwa hawatakiwi kuibua mapingamizi yasio ya msingi kwa lengo la kuchelewesha usikilizaji wa mashauri mahakamani.

Imeazimiwa pia kuwa inapolazimu, mapingamizi yawasilishwe kwa njia ambayo yataeleweka badala ya kuwasilishwa kwa lugha za kificho au mafumbo ili kuiwezesha Mahakama au Baraza na upande mwingine kuelewa msingi wa mapingamizi na kujiandaa kujibu au kukubaliana nayo.

Pamoja na kufikia makubaliano hayo, Kikao hicho kimetayarisha mikakati mbalimbali itakayosaidia kuchochea usikilizaji wa mashauri, hivyo kuharakisha utoaji wa haki kwa wakati kwa wananchi katika Mahakama hiyo.

Baadhi ya mikakati iliyopitishwa na kuanza kutelelezwa mara moja ni Mahakama kuendesha vikao vitano (5) vya kusikiliza mashauri ya mlundikano na yale yanayokaribia kuwa mlundikano kwa kuzingatia kalenda ya Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na kuondokana na maahirisho ya kusikiliza mashauri yasiyo ya lazima.

Mkakati mwingine ni barua za wito wa mashahidi kutoka Taasisi za Serikali kuandikwa na Jaji au Naibu Msajiii mhusika ili kuboresha usikilizwaji wa mashauri kwa tarehe zilizopangwa na Mahakama.

Awali Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Crecensia Kisongo aliwasilisha taarifa ya hali ya mashauri ya mwaka 2021, hali ya mashauri mpaka kufikia tarehe ya kikao na hali ya mashauri ya mlundikano mpaka kufikia tarehe ya kikao.

Msajili huyo aliwataarifu wajumbe wa Kikao hicho kuwa jumla ya mashauri 56 ya mlundikano yamepangwa kusikilizwa kwenye vikao kuanzia tarehe 14 Machi, 2022 hadi tarehe 13 Aprili, 2022 ambapo Majaji wanne wa ndani ya Divisheni ya Ardhi wataendesha vikao hivyo.

Wadau waliohudhuria Kikao hicho ni Majaji wa Mahakama Kuu -Divisheni ya Ardhi, Naibu Msajiii Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea wa chapta za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Mwakilishi wa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi,Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba wa Wilaya wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Agnes Mgeyekwa akiendesha Kikao Maalum kilichowaleta wadau mbalimbali kujadili na kupanga mikakati itakayosaidia kuondoa mashauri ya mlundikano. 
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Crecensia Kisongo akiwasilisha hali ya mashauri mbele ya kikao hicho.
Sehemu ya wadau waliohudhuria kikao hicho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni