Na. Francisca Swai – Mahakama, Musoma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amemaliza ziara
yake ya kikazi kutembelea shughuli mbalimbali za kimahakama na kuwapongeza
watumishi wote kwa kuendelea kuchapa kazi licha ya ugumu wa mazingira na
changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza
na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Musoma katika kikao
cha majumuisho siku ya mwisho, Mhe. Mtulya amesema katika ziara yake amejifunza
mambo mengi, ikiwemo moyo wa kujituma na uchapaji kazi kwa bidiii kwa watumishi
wote wa Mahakama.
“Nimejionea
ubunifu mkubwa uliofanywa na watumishi ili kuboresha mazingira ya kazi, utunzaji
wa mazingira, ukarabati wa majengo, utajiri mkubwa wa ardhi na ulinzi wa mipaka
ya maeneo ya Mahakama, ushirikiano mlionao kati ya Mahakama, wadau na viongozi
wa kiserikali,” amesema.
Mhe.
Mtulya aliwaasa watumishi kuwa huru kutoa maoni, mapendekezo na kueleza
changamoto zinazowakabili kwa viongozi ili waweze kushirikiana kuzitatua kwa pamoja.
Alisema
kwa kufanya hivyo kila mmoja wao atakuwa ametimiza wajibu wake katika kuboresha
mazingira ya kazi, kuleta ufanisi na kuisaidia Mahakama kufikia malengo yake kikamilifu
katika kumhudumia mwananchi.
Katika
kikao hicho, Mhe. Mtulya, alimtaka Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Musoma, Mhe. Frank Moshi pamoja na Mtendaji wa Kanda hiyo, Bw. Festo Chonya kushirikiana
na kuhakikisha shughuli za usikilizwaji wa mashauri zinafanyika bila vikwazo
vyovyote.
Aidha,
Jaji Mfawidhi huyo alimpongeza Bw. Chonya kwa jitihada anazofanya ndani ya Kanda
kuboresha majengo ya Mahakama licha ya ufinyu wa bajeti, ikiwemo uboreshaji wa
kuridhisha wa nyumba ya kufikia Majaji iliyoko Tarime.
Mhe.
Mtulya alimsisitizia Mtendaji huyo kuendelea na mpango uliopo wa kukarabati Mahakama zingine, kuweka alama tambuzi
kulinda mipaka ya maeneo yote ya Mahakama na kuhakikisha hati miliki za maeneo
hayo zinapatikana.
Hata
hivyo, Jaji Mfawidhi huyo alimtaka Bw. Chonya kushughulikia changamoto za watumishi
kwa wakati na kuwasilisha Makao Makuu zile zinazohitaji utekelezaji wa juu
zaidi hasa za watumishi wanaokaribia kustaafu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa nne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama, Afisa Tarafa ya Kiagata Bi, Levina Julius (wa pili kushoto) na Mtendaji wa Kata ya Mangemange, Bw. Kizito Kahaga (aliyesimama nyuma). Viongozi hao wameridhia Mahakama kuendesha huduma zake katika jengo la Ofisi ya Tarafa baada ya paa la Mahakama ya Kiagata kuezuliwa kutokana na mvua yenye upepo mkali iliypokuwa ikinyesha mwezi Desemba 2021.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mhe. Erick Marley (wa pili kulia) pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama hiyo wakipokea kwa furaha vitendea kazi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya baada ya kikao cha majumuisho ya ziara yake.Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo
Kiagata, Mhe. Kenedy Mwaikambo akisoma taarifa ya utendaji kazi mbele ya Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.
Mlinzi wa Mahakama ya Mwanzo Zanaki, Bw.
Albinus John Simeo, akimuonesha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma,
Mhe. Fahamu Mtulya jengo lililotumika kama nyumba ya Chifu Wanzagi aliyekuwa
akiamua migogoro mbalimbali ya wananchi wa eneo hilo la Zanaki/Muryaza kabla ya
kuanzishwa Mahakama ya Zanaki mwaka 1964.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni