Jumatatu, 28 Machi 2022

JAJI MZUNA ATOA UJUMBE MZITO KWA WATUMISHI AKIAGWA ARUSHA

 Na Angel Meela-Mahakama, Arusha

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna amewakumbusha watumishi wa Mahakama kuendelea kuchapa kazi na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.

Mhe. Mzuna ametoa rai hiyo leo tarehe 28 Machi, 2022 katika hafla fupi ya kuwaaga watumishi wanaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha mara baada ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, Masijala Kuu jijini Dar es Salaam.

“Wananchi ndio waajiri wetu namba moja, mwananchi ndiye anaetulipa mshahara. Mnyonge ataonewa kama viongozi hawatasimamia haki, hivyo nawaomba mtangulize maslahi ya wananchi kwanza mnapotekeleza majukukumu yenu,” amewaambia watumishi hao.

Mhe. Mzuna amemkaribisha Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama, katika Kanda hiyo, Mhe. Joachim Tiganga ambaye awali alikua Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza.

Amewasihi watumishi wote kumpa Mhe. Tiganga ushirikiano mara kumi au hata mara sabini zaidi ya waliompa yeye ili kuendelea kuing’arisha Kanda hiyo katika mambo mbalimbali ya kimahakama. Mhe. Mzuna amemhakikishia Jaji Mfawidhi huyo mpya kuwa timu nzima iliyopo katika Kituo Jumuishi Arusha inafanya kazi vizuri na kwa  ushirikiano wa hali ya juu.

Jaji Mzuna aliitumia nafasi hiyo kumpongeza Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Mohamed Gwae, kwa namna ya pekee kwa kumaliza mashauri mengi kuliko majaji wengine kwa mwaka 2021. Mhe. Gwae alimaliza mashauri zaidi ya mia tatu katika kipindi hicho, hatua iliyomfanya Jaji Mzuna kumpatia cheti cha pongezi.

Naye Jaji Tiganga amemshukuru Mhe. Mzuna kwa kazi nzuri iliyotukuka aliyoifanya wakati anaitumikia Mahakama ya Tanzania kama Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.

“Historia yangu haiwezi kukamilika bila yeye (Jaji Mzuna) kutajwa kwa sababu wakati nateuliwa kuwa Naibu Msajili, Mhe. Mzuna ndiye alikuwa Jaji Mfawidhi wangu,” alisema. Mhe. Tiganga aliwaomba watumishi wote ushirikiano katika kazi na mambo mbalimbali ya kijamii kwa vile yeye ni mgeni Arusha.

Amewapongeza Majaji kwa kazi kubwa waliyofanya, ikiwemo kupunguza mlundikano katika Kanda ya Arusha na kuomba waendelee kumpa ushirikiano huo na zaidi. Baada ya mazungumzo hayo, Mhe Mzuna alikata keki ya kuagwa na Jaji Tiganga akakata keki ya kukaribishwa kama ishara ya upendo.

 Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akifuatilia jambo katika hafla ya kumuaga iliyofanyika leo tarehe 28 Machi, 2022.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akiwa katika hafla hiyo.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akikata keki huku Mhe. Tiganga akishuhudia tukio hilo.
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (kulia) akimlisha keki Mhe. Mzuna.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna (kushoto) akimlisha keki Mhe. Tiganga.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akimlisha keki Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Bw. Leonard Maufi.


Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (kushoto) akimlisha keki Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Mohamed Gwae.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akimkabidhi cheti Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda hiyo, Mhe. Mohamed Gwae.



Maoni 1 :