Jumanne, 22 Machi 2022

TANZIA; JAJI MSTAAFU JONATHAN AFARIKI DUNIA

Marehemu Jaji Mstaafu, Mhe. Peter Mushi Jonathan enzi za uhai wake.

Uongozi wa Mahakama ya Tanzania unasikitika kutangaza kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Peter Mushi Jonathan kilichotokea tarehe 18 Machi, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Marehemu Jaji Jonathan alikutwa na umauti katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Mhe. Sarwatt ameeleza kuwa marehemu Jaji Jonathan aliteuliwa kuwa Kaimu Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 19 Aprili, 1971 na hatimaye kuthibitishwa kuwa Jaji mnamo tarehe 24 Februari, 1973.

Msajili huyo ameongeza kuwa marehemu Jaji Jonathan aliyezaliwa tarehe 14 Machi, 1934 alistaafu kwa hiari tarehe 01 Septemba, 1979.

Marehemu alishika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa Hakimu, Naibu Msajili, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama na vilevile aliwahi kuwa Kaimu Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Kudumu la Kazi (Permanent Labour Tribunal).  

Mhe. Sarwatt ameongeza kuwa mara baada ya kustaafu marehemu Jaji Jonathan alikuwa akifanya kazi ya Uwakili wa Kujitegemea hadi alipofikwa na umauti.

Taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika na anatarajiwa kuzikwa kesho tarehe 23 Machi, 2022 saa 7 mchana nyumbani kwake katika kijiji cha Mkuu Kitongoji cha Kiserenyi Tarafa ya Machame, Moshi-Kilimanjaro.

Mahakama ya Tanzania inatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia msiba huu.

BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.

 

Maoni 1 :