· Yatoa Rai vyombo vya upelelezi kuharakisha upelelezi
Na
Lydia Churi- Mahakama
Jaji wa Mahakama ya
Rufani ya Tanzania ambaye pia ni mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Gerald Ndika ametoa rai kwa vyombo vya upepelezi nchini kukamilisha uchunguzi
wa malalamiko kabla ya kufungua mashauri mahakamani.
Akizungumza kwenye
Mkutano kati ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau wa Mahakama
uliofanyika jana mkoani Pwani, Jaji Ndika ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa
Tume hiyo alisema jeshi la polisi halina budi kuharakisha upelelezi ili
kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri na kurahisisha upatikanaji wa haki.
“Kila mdau wa Mahakama
anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi kwa kuwa mfumo wa utoaji haki
unategemeana, Mahakama peke yake haitaweza kutoa haki kwa wakati endapo wadau
wake watabaki nyuma”, alisema Jaji Ndika.
Alisema kwa upande wa
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ni vema upelelezi wa maabara ukafikishwa
mahakamani kwa haraka na ukiwa ukiwa umekamilika. Jaji Ndika pia alitaka
upelelezi wa mashauri yanayowahusisha watoto kukamilika kwa haraka ili kuongeza
kasi ya upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Aidha, Kaimu Mwenyekiti
wa Tume hiyo amewataka Majaji na Mahakimu nchini kuhakikisha kuwa mashauri
yanayopokelewa mahakamani ni yale ambayo upelelezi wake umekamilika ukiacha
mashauri ya mauaji ambayo upeplelezi wake huchukua muda mrefu.
Alisema moja ya majukumu
ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ni pamoja na kufanya uboreshaji wa huduma
zinazotolewa na Mahakama hivyo ameshauri Uongozi wa Mahakama kutoa ruhusa kwa
Mahakimu wenye mamlaka ya ziaida (Extended
Jurisdiction) kutoa uamuzi kwenye mashauri ili kupunguza mlundikano wa
mashauri mahakamani.
Wakati huo huo, Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani ambaye pia ni mjumbe
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ameyataja baadhi ya mafanikio ya Mahakama ndani
ya kipindi cha miaka mitano kuwa ni pamoja na kubadilisha mfumo wa uongozi
kupitia Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 imeleta ufanisi
katika utendaji kazi wa Mhimili huo.
Jaji Siyani alisema
kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa awali wa miaka mitano 2015/2016 mpaka
-2020/2021 pamoja na mpango Mkakati mpya wa 2021/2025 Mahakama ya Tanzania imefanya
uboreshaji mkubwa wa huduma inazozitoa ikiwemo kujenga majengo ya kisasa na
kuingia kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iliyosaidia
kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama.
Kwa mujibu wa Jaji
Siyani, Mahakama katika kipindi cha miaka mitano imefanikiwa kuimarisha
uwajibikaji unaolenga kupata matokeo ambapo zaidi ya asilimia 77 ya wananchi
wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na Mahakama. Alisema Mahakama imeweka
kiwango cha chini cha idadi ya mashauri yanayopaswa kusikilizwa na Majaji na
Mahakimu kwa mwaka ambapo kila Jaji ni mashauri 220, Mahakimu wa Mahakama za
Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya mashauri 250 na Mahakimu wa Mahakama za
Mwanzo mashauri 260 kwa mwaka.
Aidha Jaji Kiongozi
alisema matarajio ya Mahakama kutoka kwa wadau wake ni pamoja na vyombo vya
upelelezi kuzingatia sheria, taratibu na miongozi ili upelelezi ufanyike kwa
haraka na kusaidia mashauri kumalizika kwa wakati mahakamani. Alishauri
kutumika kwa njia za kisayansi kukusanya ushahidi ikiwemo matumizi ya vipimo
vya Vinasaba (DNA) pamoja na ushahidi wa picha za video kwa kuwa sheria
inaruhusu.
Alisema Mahakama
inatarajia wadau wanaohusika na upelelezi kuhakikisha kuwa tuhuma za jinai zinapelelezwa
kwanza kabla ya kufikishwa mahakamani. Alisisitiza mashauri ya jinai kufunguliwa
baada ya ushahidi wa kutosha unaowezesha kufungua shauri kupatikana.
Alisema Mahakama inayo mifumo
ya kutosha kuwezesha sheria kuchukua mkondo wake na kuondokana na mlundikao wa
mashauri hivyo ametoa wito kwa wadau wa Mahakama wakiwemo wananchi kufungua
mashauri kwa njia ya mtandao kwa kuwa wanaweza kufanya hivyo ndani ya saa 24.
Jaji Kiongozi alisema Mahakama
inayo matarajio kuwa kila chombo ambacho ni mdau wake kitakuwa na Mpango Mkakati
wake utakaosaidia uboreshaji wa mnyororo wa utoaji haki. Aliwataka wadau kufanya
kazi kwa kuzingatia sheria taratibu na miongozo wanapotekeleza kwa maslahi ya Taifa
pamoja na wananchi.
Wajumbe wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama wameanza ziara katika katika mikoa ya Pwani, Morogoro na
Tanga kwa lengo la kuitangaza Tume hiyo, kutoa elimu na kukutana na wajumbe wa
Kamati za Maadili za mikoa na wilaya pamoja na wadau wa Mahakama ili kuboresha
huduma zinazotolewa na Mahakama.
Sehemu ya Wadau wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama uliofanyika jana Mkoani Pwani. Wajumbe wa Tume hiyo wameanza ziara katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Tanga kwa lengo la kuitangaza Tume, kutoa Elimu na kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau ili kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama za Mkoa na wilaya wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama uliofanyika jana Mkoani Pwani.
Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama za Mkoa na wilaya wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama uliofanyika jana Mkoani Pwani.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Gerald Ndika akizungumza wakati wa Mkutano kati ya wajumbe wa Tume hiyo na Wadau wa Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume hiyo na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama jana mkoani Pwani.Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama za Mkoa na wilaya jana mkoani Pwani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni