Na Mary Gwera, Mahakama
Watumishi wanawake wa Kada mbalimbali kutoka Mahakama ya Tanzania mkoa wa Dar es Salaam leo tarehe 07 Machi, 2022 wametoa msaada kwa Wafungwa na Mahabusu wanawake waliopo katika Gereza la Segerea jijini humo.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao kabla ya kukabidhi vitu mbalimbali kwa Mkuu wa Gereza hilo, Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bi. Mercy Mangweha amesema kuwa wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 08 Machi, kila mwaka.
“Tumekuja hapa leo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya wanawake, kama mnavyofahamu kilele cha Wiki hii ni kesho tarehe 08 Machi, 2022, hivyo tumeamua kuja kutoa misaada kwa kundi la Wanawake wafungwa na Mahabusu waliopo katika Gereza hili ili tufurahi kwa pamoja,” alisema Bi. Mercy.
Aliongeza kuwa misaada ya vitu mbalimbali waliyotoa imetokana na michango iliyotolewa na wanawake wanaofanya kazi katika Mahakama za ngazi mbalimbali mkoani Dar es Salaam kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani (T).
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Wanawake-Segerea, SP Yange Saganda aliwashukuru Watumishi hao waliowasilisha misaada kwa niaba ya wenzao, huku akisema kuwa vifaa hivyo vitatumika na kuwasaidia walengwa kama ilivyokusudiwa.
“Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuamua kuja katika Gereza hili kuwapa tabasamu Wanamama hawa, misaada hii itawasaidia pia baadhi ya Wafungwa/Mahabusu ambao hawana ndugu wa kuwaletea mahitaji mbalimbali,” alisema SP Saganda.
Vitu vilivyotolewa ni pamoja na sabuni za kufulia, dawa za meno, miswaki, ‘Pampers’, mafuta ya kujipaka na kadhalika.
Watumishi wanawake wa Kada mbalimbali kutoka Mahakama ya Tanzania mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Maafisa Magereza kutoka Gereza la Segerea wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Watumishi wa Mahakama kukabidhi vitu mbalimbali ikiwa ni msaada kwa Wafungwa/Mahabusu Wanawake waliopo katika Gereza hilo. Zoezi hilo limefanyika leo tarehe 07 Machi, 2022.
Mkuu wa Gereza la Wanawake-Segerea, SP Yange Saganda (kulia) akipokea sehemu ya msaada kutoka kwa Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bi. Mercy Mangweha (kushoto) wanaoshuhudia ni baadhi ya Watumishi wanawake wa Mahakama mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki katika zoezi hilo.
Zoezi la kukabidhi vitu mbalimbali likiendelea.
Mahakama na Magereza; Sehemu ya Watumishi wanawake wa Mahakama Mkoa wa Dar es Salaam na Maafisa kutoka Gereza la Segerea wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilika kwa zoezi la utoaji msaada katika Gereza la Wanawake.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni