Jumanne, 22 Machi 2022

UBUNIFU WA HAKIMU TARIME WAMKOSHA JAJI KANDA YA MUSOMA

 Na. Francisca Swai – Mahakama, Musoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewapongeza watumishi walioonesha uwezo wa kufanya mambo mazuri nje ya kazi zao za ajira, ikiwemo kutunza mazingira na kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama.

Katika siku yake ya nne ya ziara ya kikazi leo tarehe 22 Machi, 2022 kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama katika Kanda yake, Mhe. Mtulya amesema kuwa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini ni moja kati ya Mahakama ambazo zimefanyiwa mabadiliko makubwa kupitia ubunifu binafsi wa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Chana Mhembe Chana.

Amesema juhudi za Hakimu huyo zilitambuliwa na kupongezwa kwa kupewa cheti cha ubunifu na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda hiyo ya Musoma, Mhe. John Kahyoza.

Juhudi hizo za ubunifu zimeendelea kuonekana katika Mahakama ya Mwanzo Sirari ambapo watumishi wa kituo hicho wamejitahidi kulinda mazingira kwa kupanda miti kuzunguka eneo la Mahakama hiyo ambayo pia hutumika kama mpaka.

Aidha, Mhe. Mtulya amwelekeza Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya kumtambua na kumpongeza mtumishi msataafu ambaye aliyekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Sirari, Mhe. Pesta Chacha kwa mchango na jitihada kubwa alizofanya kusimama kidete kulinda mipaka ya eneo la Mahakama hiyo lilipotaka kuvamiwa.

Inaelezwa kuwa Hakimu huyo aliyestaafu mwezi Septemba 11, 2020 alipanda miti kuzunguka mipaka ambayo hutumika kama alama tambuzi za eneo la Mahakama hiyo hadi leo.

Katika ziara yake hiyo, Mhe. Mtulya ametembelea Mahakama za Mwanzo Mtana iliyojengwa mwaka 1956 na kufungwa mwaka 2000 kutokana na ukosefu wa mashauri kwani wananchi wengi wa eneo hilo walipendelea zaidi kutumia mabaraza ya jadi kuliko Mahakama.

Amesema kuwa kwa sasa kuna uhitaji wa Mahakama kutokana na uelewa katika jamii na ongezeko la watu shughuli za kiuchumi ikiwemo uwepo wa mnada mkubwa siku za Jumatano katika eneo hilo lililopo kilomita 13 kutoka ilipo Mahakama ya Mwanzo Tarime mjini.

Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini wakipokea vitendea kazi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati).

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini (wa pili kushoto), Mhe. Chana Mhembe Chana akielezea namna walivyofanikiwa kuwatumia wafungwa wa nje katika shughuli mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa bahasha zinazotumika kusambaza summons kwani Mahakama hiyo hupokea mashauri mengi katika Kanda ya Musoma. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akiwa katika picha ya pamoja ya viongozi wa Mahakama Kanda ya Musoma, viongozi wa Mahakama ya Wilaya Tarime na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Sirari.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akisalimiana na wafungwa wa kifungo cha nje wanaofanya shughuli za usafi katika maeneo ya nje ya Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini, ikiwemo kutengeneza bustani za maua.

Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Sirari, akiwemo Hakimu Mkazi Mfawidhi,  Mhe. Marwa Msabi (wa pili kushoto) wakipokea kwa furaha vitendea kazi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akitoa maelekezo kwa watumishi baada ya ukaguzi wa Mahakama ya Wilaya Tarime.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tarime wakisikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo katika picha).













 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni